Kwa mashabiki na wanachama wa Simba waliokuwa wanajiuliza kuhusu ukimya wa klabu yao katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya, Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, amefunguka na kuweka wazi kuwa nyuma ya pazia, viongozi wanafanya kazi usiku na mchana, huku akithibitisha rasmi ushindi wao katika vita ya kumbakisha Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Ahmed amewahakikishia Wanasimba kuwa hakuna siku inapita bila viongozi wa ngazi za juu kukutana kwenye vikao vizito vya kimkakati. Vikao hivyo, vinavyomshirikisha pia Kocha Davids, vinalenga kupanga kwa umakini mkubwa usajili wa wachezaji wapya na kuweka mikakati kabambe itakayoirejesha timu kwenye kilele cha mafanikio.
"Hatupo kimya kama wengi wanavyodhani," alisema Ahmed. "Viongozi wa juu wapo kwenye vikao kila siku. Tunajadili mustakabali wa klabu na maandalizi ya msimu ujao. Mambo yakiwa tayari, tutakuja kuwaeleza mwelekeo wetu ni upi."
Habari kubwa na ya faraja kwa Wanasimba ni kuthibitishwa rasmi kuwa Kocha Fadlu Davids ataendelea kuwa Msimbazi. Ahmed alikiri kuwa haikuwa kazi rahisi kumbakisha kocha huyo raia wa Afrika Kusini, kwani ubora wake uliwavutia vigogo wengi barani Afrika na hata Ulaya.
"Nikwambie, ilikuwa ni vita kwelikweli. Klabu kubwa kubwa barani Afrika na hata Ulaya zilikuwa zinahitaji saini ya Fadlu. Vikumbo vilikuwa vikubwa mno," alifafanua Ahmed. "Lakini yeye mwenyewe ameipenda Simba na ameona hapa ndipo mahali sahihi kwake kuendelea na kazi. Amefanya maamuzi na sasa anashirikiana na uongozi kuboresha kikosi."
Ahmed pia alitoa ramani kamili ya nini kinachofuata kwa klabu hiyo. Alisema hivi karibuni wataanza kutoa shukrani ("Thank You") kwa wachezaji wanaoondoka, kisha watatangaza wale wanaobaki. Baada ya hapo, wataanza kuwatambulisha wachezaji wapya mmoja baada ya mwingine, kabla ya timu kuelekea kwenye maandalizi ya msimu "pre-season," Tamasha la Simba Day, na hatimaye kuanza mapambano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.