Simba Yaingia Sokoni kwa Kasi, Yanasa Wazawa Kwanza Huku Ikijipanga Kimataifa

sports | Sun Jul 06 2025


Simba Yaingia Sokoni kwa Kasi, Yanasa Wazawa Kwanza Huku Ikijipanga Kimataifa

Klabu ya Simba SC imeripotiwa kuwa mbioni kukamilisha usajili wa beki wa kushoto wa JKT Tanzania, Karim Mfaume Bakari, akitarajiwa kuongeza nguvu na kumsaidia Mohamed Hussein 'Tshabalala' katika safu ya ulinzi msimu ujao. Hatua hii inaendeleza azma ya Wekundu wa Msimbazi ya kunasa wachezaji kadhaa kutoka JKT Tanzania, wakiwemo beki wa kati hodari, Wilson Nangu, na golikipa mahiri, Yacoub Suleiman.


Taarifa kutoka vyanzo vya ndani zinasema kuwa mbali na kuwalenga wachezaji hao wa maafande, Simba pia inakaribia kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji mwenye kipaji, Abdallah Kulandana, anayetoka klabu ya Fountain Gate. Ujio wa Kulandana unatokana na pendekezo la Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ambaye alivutiwa na uwezo wake katika michezo yote miwili ambayo Simba ilicheza dhidi ya Fountain Gate kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.


Usajili wa Simba umeanza rasmi baada ya kukamilika kwa kikao muhimu cha Bodi ya Wakurugenzi, kilichoongozwa na Mwenyekiti Mohamed Dewji na Makamu Mwenyekiti Murtaza Mangungu, ambacho kiliishirikisha pia Bodi ya Washauri hivi karibuni. Chanzo cha ndani ya klabu hiyo kilifichua kuwa mkakati wa awali ni kumalizana na wachezaji wazawa walioonyesha uwezo mkubwa, kabla ya kuanza kuzungumza na wachezaji wa kigeni, ingawa mazungumzo na baadhi yao tayari yameanza.


"Tunataka tusajili kwanza wachezaji wa kizawa tumalize ili tuanze kutoka nje ya nchi kusajili wageni. Hatutaki kurudia makosa ya msimu uliopita ambapo kulikuwa na changamoto nyingi za usajili," kilisema chanzo hicho, kikirejea matukio yaliyojitokeza kwa wachezaji kama Lameck Lawi, Velentino Mashaka, na Awesu Awesu, ambapo klabu ilikumbana na vikwazo vingi.


Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alithibitisha kuwa klabu imeweka mikakati ya siri kuelekea kwenye kipindi cha usajili. "Kilichomriwa ni namna gani tunavamia soko la usajili, tunaboresha vipi kikosi chetu ili tupambane zaidi. Tumefanikiwa eneo la kujenga timu, lakini tumefeli kukosa makombe yote, kwa hiyo mipango iliyopo ni kuhakikisha msimu ujao tunaongeza ubora wa kikosi ili kutwaa mataji," alieleza Ahmed.


Simba imekosa mataji yote iliyokuwa ikiyapigania msimu huu, ikiwemo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (FA Cup), na Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Matokeo haya yamechochea uongozi kuweka mikakati kabambe ya usajili ili kuhakikisha wanarejesha heshima yao na kutwaa mataji msimu ujao.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.