Baada ya kufanikiwa katika lengo la awali la kuirejesha na kuibakisha timu ya Pamba SC kwenye Ligi Kuu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ametangaza awamu ya pili ya mpango huo: kuijenga upya timu hiyo ili iwe ya ushindani na iendane na hadhi ya Jiji la Mwanza.
Akizungumza jijini Dodoma, RC Mtanda ametoa maagizo mazito kwa uongozi wa klabu hiyo, akitaka timu ifanyiwe mabadiliko makubwa kuanzia kwenye benchi la ufundi hadi kwa wachezaji. Amesema ni lazima litafutwe benchi jipya la ufundi lenye weledi, na ufanyike usajili wa nguvu utakaovutia wachezaji bora watakaoipigania timu hiyo.
"Mpango wetu wa kurejesha Pamba Ligi Kuu baada ya zaidi ya miaka 23 umefanikiwa kwa asilimia 100. Sasa tunataka kuona timu inakuwa ya ushindani mkubwa na inaendelea kubaki ligi kuu kwa heshima," alisema Mtanda.
RC Mtanda, ambaye ni mlezi wa timu hiyo, ametoa onyo kali kwa viongozi wa klabu kuhakikisha fedha zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya kuihudumia timu zinatumika ipasavyo na kwa malengo yaliyokusudiwa. Alisisitiza kuwa serikali ya mkoa ina vipaumbele vingine vingi vya maendeleo, hivyo fedha za timu lazima zitumike kwa uwazi na uadilifu.
"Nawasihi viongozi wa timu, fedha zilizotolewa zitumike kikamilifu kwa ajili ya timu. Serikali ina miradi mingi ya maendeleo inayohitaji rasilimali, hivyo hatutavumilia ubadhirifu wowote," aliongeza.
Pamba SC ilirejea Ligi Kuu msimu wa 2024/2025 baada ya kukaa nje ya ligi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili. Sasa, kwa maelekezo haya ya Mkuu wa Mkoa, inatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa ili iweze kushindana vilivyo na vigogo wa soka nchini katika msimu ujao.