Katika kile kinachoonekana kama kufungua "hazina" kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza neema ya mabilioni ya shilingi, huku ikituma ujumbe mahususi kwa vijana na waandishi wa habari kuweka kando woga na kuchangamkia fursa za mikopo ya kilimo na uvuvi. Wito huo mzito umetolewa jijini Mwanza, maarufu kama 'Rock City', ambapo imebainishwa kuwa fedha zipo na zinatolewa kwa masharti nafuu ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa.
Akizungumza katika semina elekezi iliyolenga kuwanoa wanahabari kuhusu fursa hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amefunguka na kutoa ushuhuda wake binafsi. RC Mtanda amewaasa vijana kuacha kulalamika vijiweni kuhusu ukosefu wa ajira wakati TADB imeweka mezani mabilioni ya kukuza mitaji.
"Mimi Mwenyewe Nimenufaika" Mhe. Mtanda hakuuma maneno, akiweka wazi kuwa yeye ni shuhuda wa faida za benki hiyo. Alibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 pekee, jumla ya Shilingi Bilioni 7.5 zimeshatolewa kama mikopo bila riba (interest-free loans) kwa vijana 350 waliojiunga katika vikundi 47 vya uvuvi wa kisasa.
"Ni muhimu kila kijana atambue kuwa hizi fursa ni halisi. Mimi mwenyewe nimenufaika na huduma za TADB, sasa kwanini nyinyi mshindwe? Tayari vijana wenzenu wameshaanza kurejesha zaidi ya Shilingi Bilioni 1.3, ikimaanisha biashara inalipa. Siri ya mafanikio ni kuunda vikundi vya uzalishaji mali ili kuwa na nguvu ya pamoja," alisisitiza RC Mtanda.
Mwanza: Kitovu cha 'Dhahabu' ya Majini na Ardhini Kwa upande wake, Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa, Bw. Alphonce Mokoki, ameleza kuwa benki hiyo imejipanga kimkakati kuhakikisha Kanda ya Ziwa inatumia utajiri wake wa asili. Alitaja mazao ya biashara kama pamba, kahawa, na mpunga, pamoja na sekta inayokua kwa kasi ya ufugaji wa samaki (Aquaculture), ng'ombe na kuku kama maeneo ambayo benki imewekeza nguvu kubwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwa TADB mwaka 2015, benki hiyo imekuwa 'uti wa mgongo' wa wakulima nchini kwa kukopesha zaidi ya Shilingi Bilioni 631.18 katika miradi 151. Katika 'keki' hiyo ya taifa, Mkoa wa Mwanza pekee umepata kipande cha zaidi ya Shilingi Bilioni 79.14 zilizoelekezwa kwenye miradi 61 yenye tija.
Mapinduzi ya 'Vizimba' na Wito kwa Wanahabari Afisa Masoko wa TADB, Richard Sempindu, aligusia mapinduzi yanayofanywa na vijana na wanawake kupitia ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba (cage farming) ziwani. Alibainisha kuwa mpango wa uhamasishaji umesaidia vikundi 120 na wanufaika zaidi ya 1,904 Kanda ya Ziwa, jambo linaloashiria mabadiliko ya kifikra.
Naye mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Bi. Judy Ferdinand, amewataka vijana wenzake kuacha kupoteza muda na "bea" za mitandaoni (taarifa zisizo sahihi) na badala yake wafuatilie vyanzo rasmi vya habari ili wasipitwe na fursa hizi za ukombozi wa kiuchumi.
Semina hii imekuja wakati muafaka ambapo serikali inasisitiza uchumi wa buluu na kilimo biashara kama njia kuu za kutatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini Tanzania.