Baada ya kumaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika nafasi ya 11 isiyoridhisha kwa pointi 34, uongozi wa Pamba Jiji FC ya Mwanza umeonekana kudhamiria kuirejesha heshima ya klabu hiyo kongwe. Mikakati kabambe imeanza kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye uzoefu na viwango vya juu, huku ikielezwa kuwa iko mbioni kumpata kocha mpya wa kimataifa.
Katika kuhakikisha safu ya ulinzi inakuwa imara, Pamba Jiji imefanikiwa kuinasa saini ya beki wa kushoto aliyekuwa anawika na klabu ya Fountain Gate, Amos Charls Kadikilo. Mlinzi huyo mahiri amesaini mkataba wa miaka miwili na anatarajiwa kuleta changamoto mpya na kuimarisha ukuta wa timu hiyo inayojulikana kama "TP Lindanda." Kumsajili Kadikilo ni ishara tosha kwamba Pamba Jiji haitaki mzaha katika msimu ujao wa ligi.
Mbali na Kadikilo, orodha ya wachezaji wanaohusishwa kutua jijini Mwanza ni ndefu na inajumuisha majina makubwa. Miongoni mwao ni beki wa kulia na winga raia wa Ghana, Nicolaus Gyan, ambaye ana uzoefu na soka la Tanzania baada ya kuichezea Simba SC na Fountain Gate. Pia, beki kisiki wa kati kutoka Zambia, Kabaso Chongo, anayekipiga Kabwe Warriors na ambaye aliwahi kutamba na miamba ya soka la Afrika, TP Mazembe, yumo kwenye rada za Pamba Jiji. Wengine ni John Mbise kutoka Geita Gold na mshambuliaji hatari kutoka Nigeria, Umar Abba, anayeichezea Bugesera FC ya nchini Rwanda.
Wakati hayo yakiendelea, tetesi kubwa zinahusu benchi la ufundi. Ingawa timu kwa sasa ipo chini ya kocha Fred Felix Minziro, inaelezwa kuwa Mkenya Francis Baraza yuko katika hatua za mwisho za makubaliano kuchukua mikoba ya ukocha mkuu. Baraza mwenyewe amekiri kufikia asilimia 80 ya mazungumzo na uongozi wa Pamba, akivutiwa na mipango na malengo ya klabu hiyo. "Nimevutiwa na mipango yao, uongozi umenihakikishia ushirikiano mkubwa kwa benchi la ufundi, hivyo kazi inabaki kwetu kuhakikisha timu inapata matokeo," alinukuliwa Baraza.
Akizungumzia mchakato mzima wa usajili, Afisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William, alisisitiza kuwa kila kitu kinafanywa kwa weledi chini ya mapendekezo ya benchi la ufundi. "Sisi viongozi hatuingilii mapendekezo ya makocha. Wao ndio wanaotambua mahitaji ya timu na sisi tunatekeleza," alisema William, akionyesha kuwa usajili unaofanyika ni wa kimkakati na wenye malengo.