Ronnie Stam, mchezaji wa zamani wa ligi kuu ya Uingereza (EPL) aliyewahi kukipiga na klabu ya Wigan Athletic, amejikuta matatani baada ya kufikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma nzito za kusafirisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya cocaine kutoka Amerika Kusini kwenda barani Ulaya. Dawa hizo zinakadiriwa kuwa na uzito wa takribani tani mbili.
Kwa mujibu wa gazeti la Uingereza la Daily Mail lilivyoripoti mnamo Juni 12, thamani ya soko ya dawa hizo za kulevya zinazodaiwa kusafirishwa na Stam inakadiriwa kufikia pauni milioni 48, kiasi ambacho ni sawa na takribani shilingi bilioni 157.2 za Kitanzania (kwa kiwango cha ubadilishaji cha takriban TZS 3,275 kwa pauni 1). Iwapo atapatikana na hatia, Stam anaweza kukumbana na kifungo cha hadi miaka 13 jela pamoja na faini ya pauni milioni 1.5, sawa na takribani shilingi bilioni 4.9 za Kitanzania.
Waendesha mashtaka wameeleza kuwa tukio hili linahusiana na operesheni kubwa ya usafirishaji wa dawa za kulevya iliyofanywa kati ya mwaka 2020 na 2021. Ushahidi uliokusanywa unaonyesha kuwa Stam na kaka yake, Rudi, walitumia ujumbe wa simu zilizosimbwa kuficha mawasiliano yao, wakijadili usafirishaji wa cocaine. Ujumbe huo unadaiwa kuwa na maelezo ya kina kuhusu usafirishaji huo, ikiwemo picha za dawa hizo.
Stam amekiri kuhusika kama mshirika katika usafirishaji wa kilo 20 za cocaine kutoka Brazil kwenda Ujerumani mwaka 2020, lakini amekanusha tuhuma zingine za ziada. Mahakamani, Stam amejitetea akisema kuwa mali zake zote zimetokana na mapato halali aliyoyapata wakati wa enzi zake za kucheza mpira.
Ronnie Stam alicheza kwa mafanikio makubwa katika ligi kuu ya Uingereza akiwa na klabu ya Wigan Athletic kuanzia mwaka 2010 hadi 2013. Alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda Kombe la FA mwaka 2013, ingawa hakushiriki katika mchezo wa fainali. Mbali na Wigan, Stam pia amewahi kucheza soka nchini Uholanzi na klabu ya Twente, Ubelgiji na Standard Liege, na amerejea mara mbili kuichezea klabu ya NAC Breda.
Kesi hii ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza mwezi Septemba mwaka 2023, ambapo mahakama ya Breda ilihitimisha kuwa Stam alihusika moja kwa moja katika usafirishaji wa jumla ya kilo 2,217 za cocaine. Waendesha mashtaka wamesisitiza kuwa "Stam alikuwa mtu muhimu katika operesheni hii kubwa ya usambazaji wa dawa za kulevya."
Juni mwaka jana, polisi wa Uholanzi walifanya msako katika nyumba sita na kambi moja ya magari kuhusiana na kesi hii. Katika msako huo, walifanikiwa kukamata takribani pauni 85,000 taslimu (sawa na shilingi milioni 278.3 za Kitanzania), mali tatu za kifahari, boti moja, magari matatu, saa sita za kifahari, na vito vya thamani.
Kati ya waliohusika na kesi hiyo, Stam ndiye pekee aliyeshikiliwa rumande. Ombi la wakili wake la kuachiliwa kwa dhamana lilikataliwa na mahakama, ikitoa sababu ya hofu kwamba anaweza kutorokea Dubai, ambako kaka yake, Rudi, anasemekana kukaa.