Pambano kali la kisheria limeibuka katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, baada ya upande wa utetezi kupinga vikali kitendo cha Mkemia kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwasilisha kielelezo cha dawa za kulevya aina ya heroine mahakamani.
Mvutano huo ulitokea jana, Julai 10, 2025, mbele ya Jaji Godfrey Isaya, wakati kesi ya usafirishaji wa kilo 1.02 za heroine inayowakabili washtakiwa Saidi Rashidi na George David ikiendelea. Washtakiwa hao walikamatwa eneo la Mivinjeni, Temeke, mnamo Juni 2021.
Mchezo wa kisheria ulianza pale shahidi wa upande wa Jamhuri, Mkemia Edward Dilunga, alipokuwa akitoa ushahidi wake. Alieleza jinsi alivyopokea bahasha yenye sampuli za chenga chenga zilizodhaniwa kuwa dawa za kulevya, na baada ya kuzifanyia uchunguzi, alithibitisha kuwa ni heroine. Baada ya maelezo hayo, shahidi huyo, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mafuru Moses, aliiomba Mahakama ikipokee kielelezo hicho cha dawa kama sehemu ya ushahidi wake.
Hata hivyo, upande wa utetezi, ukiongozwa na Wakili Nehemiah Nkoko, uliibua pingamizi zito, ukidai kuwa shahidi huyo hana sifa za kisheria za kuwasilisha kielelezo hicho. "Mheshimiwa Jaji, shahidi huyu si afisa wa polisi aliyekamata kielelezo hiki. Kwa mujibu wa miongozo ya Jeshi la Polisi (PGO) iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi, kuna utaratibu maalum wa nani anayepaswa kuwasilisha vielelezo mahakamani. Hivyo, tunaomba kielelezo hiki kisipokewe," alidai Wakili Nkoko.
Wakili wa Serikali, Mafuru, alijibu mapigo akisema hoja za utetezi hazina mashiko ya kisheria na zinapaswa kutupiliwa mbali. Alidai kuwa si lazima askari aliyekamata ndiye awasilishe kielelezo, na kwamba mtaalamu aliyethibitisha anaweza kufanya hivyo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Isaya aliahirisha kesi hiyo na kusema atatoa uamuzi leo, Julai 11, 2025, kuhusu iwapo kielelezo hicho muhimu kitapokewa au la. Uamuzi huo unasubiriwa kwa hamu kwani unaweza kuwa na athari kubwa kwa mwenendo mzima wa kesi hiyo.