Pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara linafunguliwa rasmi kwa mabingwa wa kihistoria, Simba SC, watakapoikaribisha Fountain Gate FC leo saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Hata hivyo, mchezo huu unatajwa kuwa na sura mbili tofauti: upande mmoja kuna Simba iliyojaa kujiamini na kiu ya kuanza msimu kibabe, na upande wa pili kuna Fountain Gate inayokabiliwa na mgogoro mkubwa wa upungufu wa wachezaji.
Kauli kutoka kambi ya Wekundu wa Msimbazi, kupitia kwa Kocha Msaidizi Selemani Matola, ni moja tu: kuanza ligi kwa kishindo. Matola amesisitiza kuwa dhamira yao msimu huu ni kunyakua ubingwa, hivyo kupata alama tatu za kwanza kwa ushindi mnono ni jambo la lazima. "Tunajua haitakuwa rahisi kwa sababu Fountain Gate walipoteza mechi yao ya kwanza, lakini sisi tumejipanga. Lengo letu ni ubingwa, na safari hiyo inaanza na ushindi," alisema Matola. Aliongeza kuwa kucheza kwenye uwanja wa Mkapa ni faida kwao, kwani ni uwanja wanaouzoea na wenye bahati nao.
Wakati Simba ikiwa na kikosi karibu kamili isipokuwa Mohamed Bajaber ambaye ni majeruhi, hali ni tete kwa wapinzani wao. Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Denis Kitambi, amekiri wazi kuwa maandalizi yao yamekuwa magumu kutokana na changamoto ya kuwa na idadi ndogo ya wachezaji walioidhinishwa kucheza. Klabu hiyo ilijaribu kuomba Bodi ya Ligi kusogeza mbele mchezo huu kutokana na matatizo ya kiufundi kwenye Mfumo wa Usajili wa Kimataifa (TMS), lakini ombi lao liligonga mwamba.
Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa Fountain Gate ikashuka dimbani ikiwa na wachezaji pungufu, jambo ambalo ni nadra kutokea katika soka la ushindani. Licha ya hayo, Kocha Kitambi amesema watajitahidi kupambana. "Tumeiangalia Simba inavyocheza, lakini tumejikita zaidi kurekebisha makosa yetu. Tunajua hatutapata nafasi nyingi, hivyo chache tutakazozipata ni lazima tuzitumie vizuri," alisema Kitambi.
Wakati Simba wakitamba kutokana na mabadiliko ya makocha kutoathiri ari ya wachezaji wao wa kimataifa, Fountain Gate wanapambana na hali halisi ya kuikabili mojawapo ya timu kubwa barani Afrika wakiwa na kikosi dhaifu.