Wakati Watanzania leo wanaungana kuadhimisha miaka 26 tangu kuondokewa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, sauti na falsafa zake kuhusu uongozi bora na vita dhidi ya rushwa zinarejea kwa kishindo, zikitoa taswira halisi ya changamoto inayoikabili nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Maneno yake yanabaki kuwa chemsha bongo nzito kwa taifa, hasa pale mzimu wa rushwa unapoonekana kutanda katika michakato ya kisiasa.
Mwalimu Nyerere hakuwahi kuchoka kusisitiza kuwa uongozi ni dhamana ya utumishi kwa wananchi, na si mradi wa kibiashara. Alionya vikali kwamba mgombea anayetumia fedha kununua kura ili apate madaraka, hawezi kamwe kuwa mtumishi wa umma. Badala yake, atatumia mamlaka yake kama fursa ya kurejesha gharama alizotumia na kujilimbikizia mali. "Uchaguzi wa rushwa si uchaguzi, ni biashara. Na nchi haiwezi kuongozwa kwa biashara ya kura," ni moja ya kauli zake kali zinazopaswa kuwazindua wapiga kura leo.
Katika maandiko na hotuba zake nyingi, Mwalimu aliitaja rushwa kama adui wa nne wa taifa, akiilinganisha na umaskini, ujinga, na maradhi. Aliamini kabisa kuwa rushwa ina nguvu ya kubomoa misingi ya haki na usawa kuliko hata vita wakati wa amani. "Huwezi kununua haki," aliwahi kusema, akieleza masikitiko yake jinsi saratani hiyo ilivyoanza kuota mizizi, na kufanya watu wenye vyeo, urafiki, au fedha kupata upendeleo usiostahili.
Onyo hili la kihistoria linaonekana kutimia leo. Hata Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, alikiri hivi karibuni kupokea malalamiko mengi kuhusu vitendo vya hongo wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya vyama. Hii inadhihirisha kuwa wosia wa Nyerere haukupitwa na wakati; ni kioo halisi cha jamii.
Ili kupambana na adui huyu, serikali yake iliweka sheria kali na kusimamia kwa umakini Azimio la Arusha lililoweka misingi ya maadili kwa viongozi. Aliamini kiongozi wa kweli anapaswa kuchaguliwa kwa sifa na uwezo wake, na si kwa ukubwa wa mfuko wake. Alitoa wito kwa wananchi kutokuuza utu na heshima yao kwa noti chache, akisema, "Ukimwuzia mtu kura yako, umempa haki ya kukutawala kama mtumwa."
Wakati kampeni za uchaguzi zikipamba moto, urithi huu wa fikra za Mwalimu Nyerere unabaki kuwa taa muhimu. Ni jukumu la kila Mtanzania kutafakari na kuchagua viongozi watakaotumikia nchi kwa uadilifu, na si wafanyabiashara watakaoinunua nchi kwa rushwa.