Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zimeanza kutoa mafunzo kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Shule Salama kwa walimu wanasihi 5,000 wa shule za awali na msingi nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Charles Mahera, aliyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi mafunzo hayo ngazi ya kitaifa kwa walimu wanasihi katika Chuo cha Ualimu Morogoro.
Alisema kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, walimu wanasihi hao kutoka shule za msingi 5,000 zilizoteuliwa kutekeleza Afua ya Mpango huo kupitia Programu ya BOOST kutoka halmashauri zote na mikoa ya Tanzania Bara watajengewa uwezo.
Dkt. Mahera alieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza zinashughulikiwa ili mazingira ya utoaji wa elimu yawe salama kwa ajili ya kuwasaidia walimu na wanafunzi kufikia malengo yao.
Alitaja maeneo muhimu nane ambayo yamepewa umuhimu, ikiwa ni pamoja na namna ya kuimarisha utoaji wa huduma ya ushauri nasaha shuleni, jinsi ya kukuza stadi za maisha za wanafunzi, na jinsi ya kutatua na kushughulikia malalamiko mbalimbali ya walimu na wanafunzi.
Dkt. Mahera alitaja eneo lingine kuwa ni namna ya kubaini na kushughulikia wanafunzi walio katika hatari ya kuacha shule, pamoja na namna ya kubaini na kushughulikia hatari wanazokumbana nazo wanafunzi wanapotoka nyumbani kwenda shule na kurudi nyumbani.
Pia, mafunzo hayo yataelekeza namna ya kuboresha utendaji kazi na kuzingatia maadili katika kazi ya ualimu, namna ya kuboresha na kuimarisha mahusiano kati ya shule na jamii, ikiwa ni pamoja na wazazi kupitia ushirikiano wa wazazi na shule.
Dkt. Mahera alitaja eneo lingine kuwa ni jinsi ya kushughulikia na kutatua unyanyasaji wa kijinsia; na jinsi ya kushirikiana na jamii kuhakikisha huduma ya chakula na lishe inatolewa shuleni.
Alisema serikali imetumia gharama kubwa kuwezesha mafunzo hayo, na hivyo anatarajia yataakuwa chachu ya kuleta tija na thamani kwa fedha zilizotumika kwa kuhakikisha mazingira ya shule yanaboreshwa ili kuwa salama na kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji uliofanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa wizara hiyo, Abdul Maulid, alisema mafunzo hayo kwa baadhi ya walimu yamefanyika na mengine yanaendelea kufanyika kwenye vituo vitano tofauti ambavyo ni Chuo cha Ualimu Klerruu, Chuo cha Ualimu Morogoro, Chuo cha Ualimu Korogwe, na Chuo cha Ualimu Tabora.