Hofu na ukimya vimetoweka, na sasa ujasiri na ushirikiano vimetawala katika Shule ya Msingi Nasholi, iliyopo Halmashauri ya Meru mkoani Arusha. Haya ni matunda ya Mpango wa Shule Salama, unaotekelezwa na Serikali kupitia Mradi wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Mpango huu, unaolenga kujenga mazingira ya elimu bora, salama, na jumuishi, umewabadilisha wanafunzi wa shule hiyo na kuwapa zana za kujilinda dhidi ya ukatili. Niwael Mbise, mwanafunzi na Mwenyekiti wa Baraza la Kupinga Ukatili wa Kijinsia shuleni hapo, anasema sasa wanajitambua zaidi.
"Kabla ya mpango huu, hatukujua aina za ukatili wala jinsi ya kuripoti. Sasa tumejengewa uwezo, tunajua haki zetu, na hatuogopi kutoa taarifa tunapoona viashiria vya ukatili shuleni au hata majumbani. Hii imetufanya tujisikie salama na kujiamini zaidi," anasema Niwael.
Mwalimu wa Unasihi wa shule hiyo, Anambora Swai, anathibitisha mabadiliko hayo. Anasema mpango huu umeimarisha uhusiano kati ya walimu, wanafunzi na hata wazazi. "Wanafunzi sasa wanashiriki zaidi darasani, hawana hofu, na mazingira ya ujifunzaji yamekuwa bora zaidi. Tumeona mafanikio makubwa," anasema Mwalimu Swai.
Kisa cha mafanikio katika Shule ya Msingi Nasholi ni sehemu ya hadithi kubwa ya kitaifa. Mpango huu wa Shule Salama unatekelezwa katika shule 3,800 nchini, ikiwa ni sehemu ya lengo la kufikia shule 6,000.
Tayari, jumla ya walimu wanasihi 3,800, walimu wakuu 3,800, na waratibu elimu kata 680 wamepatiwa mafunzo maalum ili kusimamia na kutekeleza mpango huu kwa ufanisi. Hatua hii inaonyesha dhamira ya dhati ya serikali ya kuhakikisha kuwa kila mtoto nchini anapata fursa ya kusoma katika mazingira salama na yanayomwezesha kufikia ndoto zake.