Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imedhamiria kuboresha mazingira ya elimu ili kuhakikisha usalama wa walimu na wanafunzi, na hivyo kuwezesha kufikia malengo ya kupata elimu bora.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Wilson Mahera, alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo kwa walimu washauri 5,000 kutoka shule za msingi 5,000 zilizochaguliwa kwa ajili ya kutekeleza Afua ya Mpango wa Shule Salama kupitia Programu ya BOOST. Walimu hawa wanatoka katika halmashauri zote za wilaya na mikoa yote nchini. Mafunzo hayo yalifanyika mjini Morogoro.
Dkt. Mahera alisema kuwa kwa sasa, utoaji wa elimu katika shule za awali na msingi unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Hizi ni pamoja na miundombinu duni na isiyotosheleza, kupungua kwa maadili katika jamii, ukosefu wa huduma ya chakula shuleni, utoro wa walimu na wanafunzi, malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu, na mazingira yasiyoridhisha ya ufundishaji na ujifunzaji katika baadhi ya shule. Aliongeza kuwa hali hii inathiri vibaya ubora na upatikanaji wa elimu bora.
"Ndiyo maana mafunzo haya yanalenga kuhakikisha kuwa changamoto zote zilizotambuliwa zinashughulikiwa ipasavyo. Tunataka kuweka mazingira mazuri ambayo yatawezesha ufundishaji na ujifunzaji kufanyika kwa ufanisi. Mafunzo haya yatasaidia kuimarisha huduma za ushauri nasaha shuleni na kuwajengea uwezo walimu wa kutatua na kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayotolewa na walimu na wanafunzi," alifafanua Naibu Katibu Mkuu.
Dkt. Mahera aliongeza kuwa mafunzo hayo pia yanalenga kuimarisha ujuzi, maarifa, na uwezo wa walimu katika kutekeleza mpango wa shule salama. Sambamba na hilo, walimu watafundishwa jinsi ya kutambua na kuwasaidia wanafunzi walio katika hatari ya kukatisha masomo, pamoja na kutambua na kushughulikia hatari zinazowakabili wanafunzi wanapokuwa njiani kutoka nyumbani kwenda shule na kurudi.
Alieleza kuwa mafunzo hayo, ambayo yatafanyika katika vituo vitano vikiwemo vyuo vya Ualimu vya Morogoro, Klerruu, Korogwe, na Tabora, yatawezesha kuboresha utendaji kazi na kuimarisha maadili katika kazi ya ualimu. Pia, yataimarisha uhusiano kati ya shule na jamii au wazazi kupitia ushirikiano mzuri.
"Mafunzo haya yatajikita pia katika kushughulikia na kutatua masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na kushirikiana na jamii kuhakikisha huduma ya chakula na lishe inatolewa shuleni. Ni muhimu wazazi watambue kuwa suala la kuchangia chakula kwa wanafunzi ni wajibu wao, sawa na wanavyowapatia chakula watoto wao wakiwa nyumbani, na halihusiani na mpango wa elimu bure," alisisitiza Dkt. Mahera.
Naye Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Magreth Matonya, alieleza umuhimu wa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata elimu bora ili waweze kufaulu katika elimu ya msingi na sekondari. Aliongeza kuwa watoto hawa wakishindwa kupata elimu stahiki wanaweza kuwa mzigo kwa wazazi na jamii kwa ujumla. Kwa hiyo, ni muhimu sana wawe katika mazingira salama ili waweze kusoma vizuri na kufaulu masomo yao.