"Ukumbi Umejaa Askari, Sisi Tunazuiwa" - Mvutano Kesi ya Lissu Mahakama Kuu

politics | Tue Sep 09 2025


"Ukumbi Umejaa Askari, Sisi Tunazuiwa" - Mvutano Kesi ya Lissu Mahakama Kuu

Hali ya taharuki na malalamiko imetawala katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, baada ya kundi la wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukumbana na kizuizi cha kuingia ndani ya ukumbi kushuhudia mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti wao wa Taifa. Tukio hili limetokea wakati shauri hilo nyeti likiendelea kusikilizwa.


Wafuasi hao wameeleza kusikitishwa na kitendo hicho, wakidai kuwa sababu iliyotolewa na ulinzi wa mahakama ya uchache wa nafasi ndani ya ukumbi ni kisingizio. Wamesema, kinyume chake, maeneo mengi ya kukaa yamekaliwa na maafisa wa Jeshi la Polisi walioimarisha ulinzi, badala ya kupewa kipaumbele wananchi ambao wana haki ya kikatiba kufuatilia mashauri yanayoendeshwa kwa uwazi.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wanachama hao aliyekuwa nje ya lango la mahakama alisema, "Inasikitisha kuona tunanyimwa haki yetu ya msingi. Tumefika hapa kwa amani kufuatilia kesi ya kiongozi wetu, lakini tunaambiwa ukumbi ni mdogo, wakati tukiona kwa macho yetu kuwa askari ndio wamejazana ndani. Hii si sawa na inaminya haki."


Kutokana na hali hiyo, wametoa wito kwa Mhimili wa Mahakama pamoja na Jeshi la Polisi kuheshimu kanuni ya uwazi katika uendeshaji wa mashauri. Wamesisitiza kuwa kesi zinazohusu viongozi wa kitaifa zinapaswa kuwa wazi zaidi kwa umma ili kuondoa hisia za kuwepo kwa ajenda za siri na kuhakikisha haki inatendeka na inaonekana ikitendeka kwa wote.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.