Dunia imeendelea kuitambua na kuiheshimu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama 'Makka' ya utulivu na kisiwa cha amani katika bara la Afrika ambalo mara nyingi limegubikwa na migogoro. Haya yamebainishwa wazi na kiongozi wa juu kabisa wa kidiplomasia duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Antonio Guterres, ambaye ameleza kufurahishwa kwake na ukomavu wa kisiasa uliooneshwa na taifa hili.
Kauli hiyo nzito imetolewa na Bw. Guterres wakati akimpokea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo. Katika mkutano huo uliojaa diplomasia ya hali ya juu, Balozi Kombo aliwasilisha ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenda kwa Katibu Mkuu huyo.
Guterres, ambaye anafuatilia kwa karibu mwenendo wa kisiasa barani Afrika, amesema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa (Role Model) linapokuja suala la mshikamano wa kijamii. Alirejea matukio ya hivi karibuni ya kisiasa, hususan yale yaliyojiri wakati wa uchaguzi na matukio ya Oktoba 29, 2025.
"Tanzania kama ishara ya Amani ilijaribiwa katika tanuru la kisiasa la hivi karibuni, lakini nchi hii ilifanikiwa kupitia mtihani huo wa kwanza kabisa kwa ujasiri mkubwa. Umoja wa Mataifa una duku duku la kuona Tanzania inabaki kuwa na umoja, mshikamano na kuendelea kuwa kielelezo cha utulivu," alisisitiza Guterres.
Hata hivyo, ili kuhakikisha amani hii inakuwa endelevu na isiyo na nyufa, Baraza la Umoja wa Mataifa (UNSG) limetoa ushauri wa kishujaa kwa wadau wote wa siasa nchini. Guterres amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa yenye tija na jumuishi (Inclusive National Dialogue). Lengo la mazungumzo hayo ni 'kufukua mizizi' na kushughulikia sababu kuu zilizopelekea matukio ya vurugu ya Oktoba 29, ili kuziba mianya yote inayoweza kusababisha kujirudia kwa hali hiyo siku za usoni.
Katika hatua nyingine inayoashiria ushirikiano dhabiti kati ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa, Guterres ameahidi kuwa Umoja wa Mataifa utaunga mkono kikamilifu jitihada za ndani za kutafuta ukweli. Ametoa baraka zake kwa Tume ya Uchunguzi iliyoundwa nchini Tanzania, akisisitiza kuwa UN ipo tayari kutoa ushirikiano baada ya tume hiyo kukamilisha jukumu lake nyeti la kuchunguza kiini cha vurugu hizo.
Kauli hii ya UN inakuja wakati ambapo Tanzania inaendelea kujipambanua kimataifa chini ya uongozi wa Rais Samia kupitia falsafa ya 4R (Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu na Kujenga Upya), ikidhihirisha kuwa diplomasia ya uchumi na amani ndiyo nguzo kuu ya taifa kwa sasa. Kitendo cha Tanzania kuvuka salama mawimbi ya kisiasa ya mwaka 2025 kinazidi kuipa heshima katika ukanda wa SADC na Afrika Mashariki.