Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Marekani, yamezizima kwa muda na kisha kuamka tena kwa shughuli mpya, baada ya kufungwa kwa Mkutano wa 79 na kuzinduliwa rasmi kwa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu. Pamoja na uzinduzi huo, ulimwengu ulimshuhudia Annalena Baerbock akipokea kijiti cha urais wa baraza hilo, huku akija na kaulimbiu inayohimiza umoja: "Pamoja Tunaweza Zaidi—Miaka 80 ya Kuimarika Pamoja, Miaka 80 ya Kukuza Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu."
Hata hivyo, katika hotuba yake ya kwanza kabisa, Rais Baerbock hakuonesha dalili za kusherehekea, bali aliibua maswali mazito yaliyoacha tafakari nzito. Alisema, "Mkutano huu wa 80 ni wa kipekee, unaadhimisha miaka mingi kuliko umri wa kuishi wa binadamu wengi. Tunapaswa kusherehekea, lakini je, kweli tuna moyo wa kufanya hivyo?"
Baerbock aliuchora ulimwengu uliojaa simanzi kupitia mifano hai inayoumiza. Aliwakumbuka wazazi katika Ukanda wa Gaza wanaotazama watoto wao wakifa njaa, wasichana nchini Afghanistan waliopokwa haki ya kwenda shule, na wakazi wa visiwa vya Pasifiki ambao makazi yao yanasombwa na mawimbi kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari. Hakuwasahau takriban watu milioni 808 duniani kote ambao bado wametekwa katika mtego wa umaskini wa kupindukia.
Kwa uchungu, alihoji, "Badala ya kusherehekea, watu hawa watauliza, Umoja wa Mataifa ulioanzishwa kutuokoa kutoka katika lindi la mateso uko wapi?" Licha ya ukosoaji huu mkali, alisisitiza ukweli kwamba Umoja wa Mataifa bado ndilo jukwaa pekee duniani lenye uwezo wa kuzileta pamoja serikali na watu wote ili kuchukua hatua za pamoja. Alisema sasa ni jukumu la kizazi hiki kuujenga upya, kuuboresha, na kuufanya Umoja wa Mataifa uendane na mahitaji ya miaka 80 ijayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, aliunga mkono kauli hiyo. Alikumbusha jinsi waasisi wa UN walivyokutana miaka 80 iliyopita mjini San Francisco wakiwa na lengo la kuunda chombo tofauti kitakachozuia majanga kama vita. Hata hivyo, alikiri kwa masikitiko kwamba changamoto za zamani kama umaskini, njaa, magonjwa na ukosefu wa usawa zimezidi kuwa mbaya.
Guterres alisisitiza kuwa kadiri matatizo yanavyoongezeka, ndivyo umuhimu wa Mkataba wa UN unaosisitiza maadili na kanuni za pamoja unavyozidi kuonekana. Alisema azimio la "Mkataba wa Mustakabali," lililopitishwa Septemba mwaka jana, litakuwa nyenzo muhimu ya kufufua matumaini na malengo ya awali ya UN.
Alimalizia kwa kusema kwamba Mkataba wa UN hauwezi kujitekeleza wenyewe, bali unategemea ushirikiano na kuaminiana baina ya nchi wanachama. Alitoa wito wa dharura wa kurejesha imani hiyo, akisema mikutano ya ngazi za juu itakayofanyika kati ya Septemba 22 na 30, itatoa fursa ya kujadili changamoto mpya za dunia, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na masuala ya akili mnemba (AI), ili kuadhimisha miaka 80 ya UN kwa vitendo.