Katika kile kinachoonekana kama kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa dhidi ya mwenendo wa demokrasia nchini, Taasisi ya Wakfu wa Thabo Mbeki (Thabo Mbeki Foundation), imetoa tamko nzito na la kishindo likihoji uhalali wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025. Taasisi hiyo inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, mwanadiplomasia nguli Thabo Mbeki, imeweka wazi kuwa Tanzania inahitaji "mwanzo mpya" wa haraka ili kujinasua katika kile walichokiita ni giza la kisiasa.
Kupitia risala hiyo ambayo imezua mjadala mpana katika duru za kidiplomasia, Wakfu huo umepigilia msumari kwenye ripoti za awali zilizotolewa na waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU). Taasisi hiyo imebainisha bila kumung’unya maneno kwamba, mchakato mzima wa uchaguzi huo uligubikwa na mapungufu makubwa ya kisheria na kikanuni, kiasi cha kushindwa kukidhi viwango vya kimataifa vya uchaguzi wa kidemokrasia.
Rambirambi na Kilio cha Haki Kabla ya kutoa nondo zake za kisiasa, Wakfu huo ulianza kwa kugusa nyoyo za Watanzania kwa kutoa pole na rambirambi za dhati kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika vurugu zilizochagizwa na joto la uchaguzi huo. "Tunatoa pole kwa damu iliyomwagika," sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka, ikisisitiza kuwa thamani ya uhai wa Mtanzania haipaswi kupotea kwa sababu ya sanduku la kura.
Hoja kuu ya Wakfu huo imejikita katika uhalisia wa matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kwa mujibu wa taasisi hiyo, ikirejea ripoti za SADC na AU, matokeo hayo "hayaakisi dhamira na mapenzi ya kweli ya mpigakura wa Tanzania." Wameeleza kuwa mazingira ya uchaguzi yaliwanyima wananchi uhuru wa kuchagua viongozi wao, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora ambayo Tanzania imekuwa ikijivunia kwa miongo kadhaa kama kisiwa cha amani.
Diplomasia ya 'Rafiki wa Kweli' Akifafanua msimamo huo, Wakfu wa Thabo Mbeki umesisitiza kuwa unatoa maoni hayo si kwa nia mbaya, bali kwa msingi wa urafiki wa damu uliopo kati yao na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Historia inaonyesha kuwa Thabo Mbeki amekuwa rafiki wa karibu wa Tanzania, nchi ambayo ilikuwa kimbilio la wapigania uhuru wa Afrika Kusini. Hivyo, tamko hili linatafsiriwa kama ushauri wa "mzee kwa mwanae" au "rafiki kwa rafiki" anapoona mwenzake anakwenda mrama.
Wito wa Mazungumzo ya Kitaifa Katika kutafuta dawa ya kudumu ya mpasuko huu, Wakfu huo umeshauri kuwa njia pekee ya kuponya majeraha ya taifa ni kupitia ukweli na uwazi. Wamependekeza kuitishwa kwa Mazungumzo ya Kitaifa (National Dialogue) yatakayohusisha pande zote bila ubaguzi.
"Hatuwezi kufikia maridhiano ya kweli kama tutaficha ukweli wa kilichotokea. Tanzania inapaswa kujiuliza maswali magumu: Nini kilikosekana? Wapi tulijikwaa? Na nini kifanyike kurejesha umoja wa kitaifa?" ilisisitiza taarifa hiyo.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanatafsiri tamko hili kama kengele ya hatari kwa Tanzania, ikizingatiwa kuwa linatoka kwa taasisi yenye heshima kubwa Barani Afrika. Wakfu huo umehitimisha kwa kusema kuwa matokeo chanya na kurejesha hali ya kawaida hakuwezi kuletwa kwa mabavu, bali kwa kukaa meza moja na kukubaliana kuwa nchi ni kubwa kuliko makundi ya kisiasa.