Mgombea urais kupitia Chama cha UDP, Saumu Rashid, ameweka wazi dira ya serikali yake endapo atapata ridhaa ya kuongoza Tanzania, akiahidi sera ya mapinduzi ya viwanda na kilimo inayolenga kumwezesha kila Mtanzania kiuchumi. Akihutubia wakazi wa kata ya Chang'ombe jijini Dodoma leo, Bi. Rashid alisema falsafa kuu ya chama chake ni "kuwajaza mapesa Watanzania," na njia ya kufikia lengo hilo ni kupitia uwekezaji wa kimkakati.
Alifafanua kuwa serikali yake itatekeleza mpango kabambe wa "Kiwanda Kila Mkoa," ambapo kila mkoa utajengewa kiwanda kitakachozingatia aina ya rasilimali inayopatikana kwa wingi katika eneo husika. Alisema mkakati huu utafungua fursa nyingi za ajira, utaongeza thamani ya mazao na maliasili, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanasambaa nchi nzima badala ya kujikita mijini pekee.
Akitolea mfano Mkoa wa Dodoma, Bi. Rashid aliahidi kuwainua wakulima wa zabibu ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya soko na hasara kutokana na mazao yao kuharibika mashambani. "Tutaweka mkazo maalum katika kuinua sekta ya kilimo cha zabibu hapa Dodoma. Tutaanzisha viwanda vya kisasa vya kutosha vya usindikaji wa mvinyo utakaouzwa ndani na nje ya nchi, ili kuhakikisha mkulima anapata faida halisi kutokana na jasho lake," alieleza.
Ili kufanikisha hili, aliongeza kuwa serikali yake itawekeza katika kupata wataalamu wa kilimo, kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, na kufanya upimaji wa udongo nchi nzima ili kilimo kiwe cha kisasa na chenye tija.
Mbali na uchumi, mgombea huyo wa UDP aligusia sekta ya afya, akiahidi kuanzisha mfumo wa huduma za afya kwa wote. Alisema chini ya uongozi wake, kila Mtanzania atapata huduma bora za matibabu bila kujali hali yake ya kiuchumi, mahali alipo, au itikadi yake ya kisiasa, akisisitiza kuwa afya bora ni msingi wa taifa lenye nguvu na lenye uwezo wa kuzalisha.