Akiwa katika Mkoa wa Simiyu, unaosifika kwa kilimo cha pamba, mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ametangaza dhamira ya serikali yake kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini endapo atapata ridhaa ya wananchi. Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Bariadi, Doyo alieleza kuwa mfumo wa sasa unamkandamiza mkulima na umefika wakati wa mabadiliko ya kweli.
Moja ya ahadi zake kuu ni kuunda mfumo wa soko huria na shirikishi, ambao utampa mkulima uhuru kamili wa kuuza mazao yake mahali popote anapotaka. Alisema serikali yake itapiga marufuku utaratibu wa sasa ambapo serikali inalazimisha kununua au kukopa mazao ya wakulima, akitaja vitendo hivyo kama unyang'anyi unaofichwa kwenye kivuli cha sheria. Alisisitiza kuwa mazao kama mbaazi na dengu yataachwa kwenye soko la ushindani bila serikali kuingilia kati.
Aidha, Doyo alitangaza wazi mpango wake wa kuvunja Bodi ya Pamba, akidai kuwa imeshindwa kutimiza jukumu lake la kuvutia wawekezaji wenye tija. Badala yake, alisema bodi hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa maslahi ya walanguzi, ambao mwishowe huwanyonya wakulima na kudidimiza bei ya zao hilo muhimu la biashara. Vilevile, aliahidi kuukomesha mfumo wa stakabadhi ghalani, akiuita kuwa ni wa kinyonyaji na unaowanufaisha madalali badala ya wakulima wenyewe.
Akihitimisha hotuba yake, Doyo aligusia suala la uzalendo, akisema haiingii akilini kuona wakulima wazalendo wakimwaga jasho mashambani, halafu faida ya kazi yao inachukuliwa na walanguzi. “Haiwezekani! Sisi katika NLD tutaiongoza nchi hii kwa misingi ya uzalendo, haki, na maendeleo ya kweli kwa kila Mtanzania," alisema Doyo, akiahidi kuwa sera za chama chake zinalenga kumkomboa mwananchi wa kawaida na kuhakikisha anapata thamani halisi ya jasho lake.