Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, imezindua mafunzo maalum ya kuongeza ujuzi na weledi kwa wakulima na wasindikaji wadogo wa mazao ya kilimo, ikiwa na lengo la kuwafikia wakulima wapatao 1,000 nchini. Lengo kuu ni kuimarisha mnyororo wa thamani ili mazao ya kilimo yachangie zaidi katika uchumi wa taifa.
Akifungua mafunzo hayo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus, aliwasihi washiriki, hususan wakulima wadogo na wasindikaji wa zabibu, kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya. Aliwakumbusha kwamba wanatakiwa kutumia ujuzi huo mpya ili kuongeza ubora wa bidhaa zao na kuboresha huduma katika sekta ya kilimo.
"Dhamira kuu ya mafunzo haya ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kuimarisha njia za utendaji kazi bora, na hatimaye kuongeza ubora wa bidhaa zetu na huduma katika sekta ya kilimo," alieleza Zuhura Yunus. Alisisitiza kuwa ingawa wakulima na wazalishaji wadogo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na malighafi kwa viwanda, wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa ujuzi wa kuongeza thamani.
Mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo. Alana Nchimbi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, mafunzo haya yatatolewa katika mikoa minne. Mikoa hiyo na mazao yanayohusika ni: Dodoma (Zabibu), Singida (Alizeti), Iringa (Nyanya na Mchicha Lishe), na Mbeya (Maharage na Parachichi). Jumla ya wakulima 250 kutoka kila mkoa watafaidika moja kwa moja na mpango huu unaoratibiwa chini ya Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Up-Skilling training).
Kwa niaba ya washiriki, Mary Uguzi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia ujuzi wenye tija. Naye Noha Madeje alibainisha kwamba wamejifunza mbinu nyingi mpya, hasa katika utengenezaji bora wa divai (wine) kutokana na zao la zabibu. Hata hivyo, wanufaika hao waliomba Serikali kuendelea kuwapatia mikopo itakayowawezesha kukuza biashara zao.
Dk. Thomas Bwana, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ambaye anaongoza timu ya wataalam wanaotoa mafunzo, aliwashauri wakulima kutumia elimu na ujuzi watakaoupata kwenda kuwafundisha wenzao. Alisema hili ni muhimu ili tija inayokusudiwa ya kuongeza ufanisi katika sekta ya kilimo iweze kufikiwa kitaifa. Dk. Bwana aliongeza kuwa TARI imejipanga kuhakikisha matokeo ya tafiti za kilimo zinawafikia na kuwasaidia moja kwa moja wakulima na wasindikaji wa bidhaa za kilimo nchini, hivyo kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Viwanda na ustawi wa wakulima.