Mwigulu Avunja Ukimya Singida: "Mke Wangu ni Neema, Sina Mabasi ya Ester Wala Biashara"

politics | Fri Nov 21 2025


Mwigulu Avunja Ukimya Singida: "Mke Wangu ni Neema, Sina Mabasi ya Ester Wala Biashara"

Katika kile kinachoonekana kama kuzima 'moto wa kifuu' uliokuwa ukiwaka chini kwa chini mitaani na mitandaoni, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ameamua kufunguka na kuweka hadharani ukweli kuhusu mali zake na familia yake. Akiwa nyumbani kwao mkoani Singida, Dk. Mwigulu amekanusha vikali uvumi uliokithiri unaodai kuwa yeye ndiye mmiliki wa kampuni maarufu ya usafirishaji ya mabasi ya 'Ester'.


Ufafanuzi huo ameutoa leo, Novemba 21, 2025, mbele ya bahari ya wananchi waliofurika katika Viwanja vya Bombadia, Manispaa ya Singida. Kwa muda mrefu, kumekuwa na maneno ya mitaani yakidai kuwa vigogo wa serikali huficha mali zao kwa majina ya watu wengine, na safari hii, Dk. Mwigulu amehusishwa na umiliki wa mabasi hayo kwa kisingizio kuwa jina "Ester" linahusiana na mkewe au mama yake.


Ukoo wa 'Mama Asha' na 'Mama Neema'


Akizungumza kwa uchungu na msisitizo huku akishangiliwa na wananchi wa nyumbani, Dk. Mwigulu amewataka Watanzania kuacha tabia ya "kumeza" kila wanachoambiwa bila kuchuja. Ametumia jukwaa hilo kutambulisha rasmi majina ya wapendwa wake ili kuondoa mkanganyiko huo uliotengenezwa na wazushi.


"Siku hizi watu wameishiwa hofu, wanazusha jambo bila hata kufanya utafiti. Nimesikia maneno eti 'Mabasi ya Ester ni ya Mbunge wa Iramba, ameyaita Ester kwa jina la mke wake'. Ndugu zangu, naomba niweke wazi hapa Bombadia; mke wangu wa ndoa haitwi Ester, anaitwa Neema," alifafanua Dk. Mwigulu.


Aliendelea kubomoa hoja za wazushi kwa kugusia upande wa wazazi wake: "Wengine wakikosa pa kushika wanasema basi yatakuwa ya mama yake. Mama yangu mzazi ni binti wa Kiislamu, anaitwa Asha Ramadhani Mohamed. Sasa huyo Ester anatoka wapi katika familia yangu?"


Miiko ya Kifugaji na Uwekezaji wa 'Watu'


Katika hali ya kuonyesha uhalisia wa maisha yake, Dk. Mwigulu alirejea kwenye asili yake ya ufugaji katika maeneo ya Iramba. Alieleza kuwa malezi na makuzi yake hayakumjenga kuwa mfanyabiashara wa vitu, bali mtumishi wa watu. Alitumia mfano hai wa mila za kwake ambapo baadhi ya biashara zinaonekana kama mwiko.


"Mimi nimezaliwa na kukulia kwenye familia ya kifugaji. Kwetu sisi, kuna vitu ambavyo haturuhusiwi kufanya kibiashara, hata kuuza miwa ni aibu. Hivyo sijawahi kuwa mfanyabiashara. Tangu nimeingia serikalini, sijawekeza kwenye mabasi wala majumba ya kifahari," alisisitiza.


Badala ya biashara, Dk. Mwigulu alibainisha kuwa "tajiri" yake ipo kwa watu. Alifichua kuwa uwekezaji mkubwa anaoufanya kwa sasa ni katika sekta ya elimu kwa watoto wasiojiweza.


"Uwekezaji wangu mkubwa ni kusomesha. Ninalo kundi la watoto zaidi ya 500 ninaowasomesha kwa fedha zangu kuanzia ngazi za chini hadi vyuo. Huko ndiko nilikoamua kuwekeza, kwenye huduma za watu na sio vyuma vya barabarani," alihitimisha huku akipigiwa makofi ya kuungwa mkono.


Kauli hii ya Waziri Mkuu inatarajiwa kuzima minong'ono ambayo imekuwa ikisambaa kwa kasi, hususan nyakati za siasa, na kuwapa wananchi picha halisi ya viongozi wao na maisha yao nje ya ofisi za umma.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.