Katika hatua ya kushangaza yenye lengo la kuponya majeraha ya kitaifa na kurejesha utulivu, Serikali ya Awamu ya Sita imeliagiza Jeshi la Polisi nchini kuweka 'mpira kwapani' na kusitisha mara moja msako dhidi ya Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Dkt. Josephat Gwajima. Agizo hili zito limetolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, likilenga kumpa nafasi kiongozi huyo wa kiroho kurejea madhabahuni kuwahudumia waumini wake baada ya msamaha uliotolewa kwa kanisa hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili, Novemba 30, 2025, na Waziri Mkuu, Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa Magufuli Leganga, uliopo Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, mkoani Arusha. Dk. Mwigulu amesema kuwa wakati wa kunyoosheana vidole umepita na sasa ni wakati wa 'Maridhiano' kwa vitendo.
Gwajima Arejee Uraiani "Rais Dk. Samia, kwa mamlaka yake na kwa roho ya kibinadamu, ameagiza vyombo vya dola viache kumtafuta Askofu Gwajima kama ilivyotangazwa awali. Waumini wake wanamhitaji, jamii inamhitaji. Mwacheni ajitokeze hadharani, aendelee na kazi yake ya kuchunga kondoo," alisisitiza Waziri Mkuu huku akishangiliwa na umati huo.
Aliongeza kuwa serikali imeshakutana na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), viongozi wa dini nyingine, na wazee wa mila ili kujenga mwafaka wa kitaifa. "Twendeni sote kwenye jambo hili, tujitokeze tuhamasishe Tanzania yenye amani. Huu ndio wito wa kiongozi wetu wa nchi; hatutaki kuona Watanzania wakiishi kwa hofu," aliongeza.
Arumeru Yaugulia Maumivu ya Vurugu Kabla ya mkutano huo wa hadhara, Waziri Mkuu Mwigulu alifanya ziara ya ukaguzi iliyojaa simanzi katika maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29. Alishuhudia mabaki ya majengo yaliyoteketezwa kwa moto, ikiwemo Kituo cha Polisi cha Kikatiti, Mahakama ya Mwanzo ya Maji ya Chai, na Kituo cha Mafuta cha Total Energies. Uharibifu huo ulihusisha pia uporaji wa mali katika maduka makubwa (supermarkets) na kuvunjwa kwa sefu za fedha, vitendo ambavyo vimeacha hasara ya mabilioni.
"Nimekuja kuwapa pole sana wananchi wenzangu wa Arumeru. Rais anaumia sana anapoona kazi kubwa ya kujenga taifa inaharibiwa kwa siku moja kwa sababu ya mihemko. Tukichagua vurugu, tunachagua umaskini. Tukichagua fujo, tunafukuza maendeleo ambayo yameahidiwa kwenye Ilani ya CCM kama maji na barabara," alionya Dk. Mwigulu.
Bilioni 4.5 na Siri ya Uranium Katika kile kilichoonekana kama kufichua 'mzizi wa fitina', Waziri Mkuu Mwigulu aliwaasa Watanzania kukataa kutumiwa kama daraja la kuvuruga nchi yao kwa maslahi ya mabeberu. Alifichua kuwa kuna taarifa za kiintelijensia zinaonyesha baadhi ya vijana na wanaharakati walioko nje ya nchi wamelipwa Dola za Marekani milioni mbili (sawa na Shilingi Bilioni 4.5) ili kupandikiza chuki na kuchochea machafuko.
"Hawa wanaowalipa hizi bilioni, wana ajenda gani na sisi? Wanataka tugombane ili wao wapate mwanya wa kuiba rasilimali zetu. Wamebaini kuwa Tanzania imegundua madini ya Urani (Uranium) yenye tani za ujazo 890,000, tukiwa nchi ya tisa duniani na ya kwanza Afrika. Wanamezea mate gesi yetu na madini adimu (rare earth minerals)," alifoka Waziri Mkuu.
Alisisitiza kuwa mbinu hii ya "wape silaha wauane, sisi tuchukue mali" imetumika katika nchi nyingi za Afrika na kuziacha zikiwa magofu. "Wanajua miradi hii ya gesi na madini ikianza, Tanzania itakuwa taifa tajiri Afrika Mashariki, hatutahitaji hata kukopesha wanafunzi, elimu itakuwa bure kabisa. Ndio maana hawataki tutulie."
Ujumbe kwa Wakulima wa Nyanya Akihitimisha hotuba yake, Dk. Mwigulu aliugusa uchumi wa mwananchi wa kawaida wa Arumeru. Aliwakumbusha kuwa vurugu hazina macho; zikitokea, hata mkulima wa nyanya na karoti kule Ngarenanyuki hatapata soko, na uchumi wa mtu mmoja mmoja utaporomoka.
"Watanzania tuamke, tukatae kurejeshwa nyuma. Amani ndio mtaji wetu mkuu. Bila amani hakuna ajira, hakuna biashara, na hakuna maisha," alimalizia Dk. Mwigulu huku akiacha ujumbe mzito wa kutafakari kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini.