Pambano la kisheria kati ya Kanisa maarufu la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, na Serikali linatarajiwa kuanza kusikilizwa rasmi Jumatatu ijayo, Julai 14, 2025, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Awali, kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa jana, lakini iliahirishwa kutokana na mwingiliano wa shughuli za kimahakama.
Kanisa hilo, kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala, limewasilisha maombi ya dharura (kesi namba 13189 ya mwaka 2025) dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Msajili wa Taasisi za Kiraia. Lengo kuu la maombi hayo ni kuiomba Mahakama itoe amri ya muda ya kusitisha zuio la serikali, ili kuruhusu waumini kuendelea na ibada na shughuli nyingine za kidini wakati wakisubiri usikilizwaji wa rufaa yao kuu.
"Maombi yetu ya amri ya muda yalikuwa yasikilizwe leo (jana), lakini sasa yatasikilizwa Jumatatu. Tunaamini Mahakama itatenda haki," alisema Wakili Kibatala.
Kesi hii imevuta hisia za wengi, huku takriban maaskofu 500 kutoka madhehebu mbalimbali wakijitokeza mahakamani katika tarehe ya awali ya kusikilizwa kwake, Juni 13, 2025, kuonyesha mshikamano na Kanisa hilo.
Mzozo huu ulianza baada ya serikali kusitisha shughuli za kanisa hilo, ambalo kiongozi wake, Askofu Gwajima, pia ni Mbunge wa Kawe. Serikali inadai kuwa kanisa hilo limekuwa likiendesha shughuli zake kinyume na masharti ya usajili, ikidaiwa kuwa baadhi ya shughuli zake zimekuwa na mwelekeo wa kisiasa kupita kiasi, jambo ambalo ni kinyume na malengo yake kama taasisi ya kidini. Sasa, Mahakama Kuu ndiyo itakayoamua hatua za awali za mzozo huu.