Lissu Alipuka Mahakamani: 'Niko Gerezani, Hata Nyie Mmeshindwa Kulinda Haki!'

politics | Thu Oct 16 2025


Lissu Alipuka Mahakamani: 'Niko Gerezani, Hata Nyie Mmeshindwa Kulinda Haki!'

Mvutano mkali na hisia za wazi zilitawala katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kutoa kauli nzito mbele ya jopo la majaji watatu, akieleza masikitiko yake juu ya kile alichokiita kushindwa kwa mahakama kulinda haki na uhuru katika kesi yake ya uhaini. Akiwa amesimama kizimbani, Lissu alilalamika kwa uchungu, akisema anajiona kama mtu aliyeko gerezani asiye na uwezo wowote, huku mahakama ikiwa imeshindwa hata kuhakikisha watu wanapata fursa ya kuhudhuria na kusikiliza kesi yake.


Akiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Lissu alieleza jinsi wafuasi wake na hata waangalizi wa kimataifa wamekuwa wakikumbana na vizingiti kila wanapojaribu kuingia mahakamani. "Tangu mwanzo wa kesi hii nimekuwa nikiieleza mahakama jinsi watu wanavyozuiwa. Hivi majuzi, baada ya kuahidiwa kuwa wataruhusiwa, walikamatwa na maafisa wa Uhamiaji na kufukuzwa nchini," alisema Lissu, akirejelea tukio la raia wa Ujerumani na Marekani. Aliongeza kuwa hii si mara ya kwanza, kwani wageni kutoka Kenya nao waliwahi kufukuzwa kwa mtindo huohuo.


Kwa hisia kali, Lissu alikumbushia historia, akilinganisha hali ya sasa na enzi za ukoloni. "Mwaka 1958, wakati wa kesi ya uchochezi ya Mwalimu Nyerere, wakoloni hawakuwazuia watu kuingia mahakamani. Hata Afrika Kusini wakati wa kesi kubwa ya uhaini mwaka 1959, serikali ya makaburu haikufanya hivi. Leo, miaka 64 baada ya uhuru, tunashuhudia mambo ya ovyo kuliko hata ya wakoloni," alilalamika Lissu. Alisema hana la kufanya zaidi ya kuweka ukweli huu kwenye kumbukumbu za mahakama ili historia isimhukumu kwa kukaa kimya.


Baada ya malalamiko hayo, Lissu aliendelea na jukumu la kumuhoji shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi John Kaaya. Katika mahojiano hayo, Lissu alimbananisha shahidi huyo kuhusu ushahidi muhimu wa video. Alimuuliza iwapo maelezo aliyoyatoa mahakamani kuhusu video hiyo, kama vile Lissu kuvaa kombati, aliyaandika kwenye maelezo yake ya awali polisi, shahidi alijibu "Sikuandika."


Lissu aliendelea kumchambua, akimuuliza kama "flashi" yenye video hiyo imewasilishwa mahakamani kama kielelezo. Shahidi alikiri kuwa bado hajaiwasilisha, jambo lililomfanya Lissu aulize, "Kwa hiyo ni sahihi nikisema hakuna aliyeiona isipokuwa wewe, hata majaji na mawakili wa serikali?" Shahidi alikubali kuwa ni kweli. Cha kushangaza zaidi, shahidi huyo alikiri kuwa hajaiangalia vizuri hati ya mashtaka na hivyo hajui kwa undani mashtaka yanayomkabili Lissu. Kesi hiyo imeahirishwa na itaendelea tena leo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.