Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete, ameweka wazi msimamo wake kuhusu kinyang'anyiro cha urais, akisema hakuna mwanasiasa yeyote nchini anayeweza kulinganishwa na mgombea wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kwa vigezo vya uzoefu, uwezo na utendaji. Akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika katika uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM kwenye viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam leo, Dk. Kikwete amesema Rais Samia amethibitisha uwezo wake kupitia matendo makubwa aliyoyafanya tangu aingie madarakani.
Dk. Kikwete alifafanua kuwa Rais Samia alikabiliwa na changamoto tatu kuu alipoingia madarakani: janga la UVIKO-19, kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wake, na haja ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Amesema kiongozi huyo alikabiliana na yote kwa ujasiri na ubunifu wa hali ya juu.
Alianza kwa kumsifu kwa kubuni Falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko, na Kujenga Upya), ambayo alisema imerejesha utulivu wa kisiasa na kuleta mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Kuhusu janga la UVIKO-19, Dk. Kikwete alieleza jinsi Rais Samia alivyotumia kwa busara fedha za msaada kutoka Benki ya Dunia. "Wakati nchi nyingine zilitumia fedha hizo kutoa ruzuku kwa wafanyabiashara, yeye alizielekeza moja kwa moja kwa wananchi kwa kujenga madarasa, vituo vya afya na kuboresha huduma za jamii. Hii ni hekima ya kipekee," alisema Dk. Kikwete.
Aidha, aligusia namna Rais Samia alivyopambana kuhakikisha miradi mikubwa kama Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma na Daraja la Magufuli inaendelea na kukamilika, licha ya baadhi yake kutokuwa na bajeti kamili. "Kwa uhodari wake, alitafuta fedha na sasa miradi hii inakwenda kwa kasi kubwa kuliko ilivyotarajiwa. Huyu ndiye kiongozi tunayemhitaji," alisisitiza Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM.