Akimpa nguvu mpya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, ameweka wazi kuwa chama hicho na wafuasi wake hawatofanya makosa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Akizungumza kwa hisia kali mbele ya umati uliofurika mjini Kibaha mnamo Septemba 28, 2025, Dk. Kikwete alitumia msemo maarufu wa "kuchanganya pumba na mchele" kusisitiza msimamo wao.
"Kamwe hatuko tayari kufanya biashara ya kuchanganya pumba na mchele. Tunajua fika madhara yake na hatuthubutu hata kujaribu," alisema Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM, akimaanisha kuwa wapiga kura wanajua kutofautisha kati ya uongozi thabiti wa CCM na wagombea wengine. Alisema hii ndiyo sababu wanaomba kura za "ndiyo" mara tatu: kwa Rais, Mbunge, na Diwani wa CCM.
Katika hotuba yake, Dk. Kikwete alimwelezea Dk. Samia kama kiongozi shupavu na mwenye afya njema anayeendelea kuchapa kazi bila kuchoka kusaka kura kote nchini. Alimpongeza kwa kuiongoza nchi kwa weledi, akimtaja kama "mama mwema" anayejali kwa dhati changamoto za wananchi wake na ni mwepesi katika kufanya maamuzi ya kuleta ufumbuzi.
Aliendelea kusisitiza kuwa chini ya uongozi wa Dk. Samia, Tanzania imesalia kuwa kisiwa cha amani na utulivu. "Tuna makabila zaidi ya 120, watu wa rangi tofauti na dini mbalimbali, lakini hakuna chuki wala mifarakano. Muungano wetu umebaki imara na ni mfano wa kuigwa barani Afrika," alieleza Dk. Kikwete, huku akisisitiza kuwa utulivu huu ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanayoonekana nchini.
Akihitimisha hotuba yake kwa ahadi nzito, Dk. Kikwete alimhakikishia Dk. Samia kuwa mkoa wake wa nyumbani, Pwani, utamlipa fadhila kwa kumpa kura nyingi za kihistoria. "Kwa wema wako na kazi kubwa uliyoifanya, tutakujazia kura nyingi kwenye masanduku mpaka zifurike. Ushindi wako unaanzia hapa," aliahidi Dk. Kikwete huku akishangiliwa na umati.