Mbunge wa Bukoba Vijijini, Dk. Jasson Rweikiza, ametoa pongezi kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne madarakani, akisema kuwa kipindi hicho kimejaa mafanikio makubwa, hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini. Dk. Rweikiza, ambaye pia ni Mwenyekiti na Mwanzilishi wa shule za St Anne Marie Academy, amesema Rais Samia ameonyesha uongozi imara kwa kusimamia na kukamilisha miradi muhimu ambayo inawanufaisha wananchi moja kwa moja.
Alieleza kuwa wakati Rais Samia anaingia madarakani, miradi mingi ilikuwa katika hatua za awali za utekelezaji, kati ya asilimia 30 hadi 40. "Mara nyingi, viongozi wapya hupuuza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wao, lakini Rais Samia amesimamia na kuhakikisha inakamilika. Sasa Watanzania wanafaidika na huduma mbalimbali kupitia miradi hii," alisema Dk. Rweikiza.
Katika sekta ya afya, Dk. Rweikiza amesema kumekuwa na maendeleo makubwa. Hospitali za mikoa na wilaya zimeimarishwa kwa kupatiwa vifaa tiba na dawa za kutosha, na hospitali za rufaa sasa zinatoa huduma za kibingwa ambazo hapo awali zilihitaji wananchi kusafiri nje ya nchi. "Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Mifupa MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma sasa zinatoa huduma za kiwango cha juu, jambo ambalo limepunguza gharama na usumbufu kwa wananchi," alieleza.
Maendeleo pia yameonekana katika sekta za elimu, nishati, na miundombinu, ambapo Tanzania inaendelea kuwa mfano wa nchi inayopiga hatua kubwa za maendeleo, na kuvutia mataifa mengine kuja kujifunza.
Mbali na mafanikio ya ndani, Dk. Rweikiza amesema Rais Samia amefanikiwa kurejesha na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na jumuiya za kimataifa, ambao hapo awali ulikuwa umedorora. "Juhudi zake zimesababisha Tanzania kuwa na mahusiano mazuri na mataifa makubwa kama Marekani, na mwaliko wake kushiriki mkutano wa mataifa yaliyoendelea duniani (G20) Januari mwaka huu nchini Brazil ni ushahidi wa heshima kubwa anayopata kimataifa," alisema Dk. Rweikiza.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, hatua hizi zinaonyesha wazi kuwa Rais Samia ameipeleka Tanzania katika kiwango kingine cha maendeleo na ushawishi wa kidiplomasia, jambo ambalo litaendelea kuleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.