Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Husna Sungura, amewahakikishia wananchi wa Jimbo la Chamanzi kuwaletea maendeleo ya kweli endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi ujao. Husna ametoa ahadi hizo mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea ubunge kupitia chama cha ACT Wazalendo.
Akizungumza kwa shauku, Husna amesema kuwa atahakikisha wananchi wa Chamanzi wanapata huduma muhimu kama umeme wa uhakika, maji safi na salama, pamoja na ukarabati wa barabara zinazowasumbua kwa muda mrefu. “Kilichonisukuma kuwania ubunge ni kuona jinsi ambavyo serikali imeshindwa kutatua kero za wananchi kwa muda mrefu. Mimi ni mzaliwa na mkazi wa hapa, ninajua changamoto wanazopitia wakazi wa Chamanzi. Nitahakikisha kila mwananchi anafaidi keki ya taifa,” alisema Husna kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa anagombea nafasi hiyo kwa nia ya dhati ya kuwahudumia wananchi na kuhakikisha kuwa kero ndogondogo zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu. “Nitapigania maendeleo ya Chamanzi kwa nguvu zote. Sitakuwa mbunge wa maneno tu, bali mbunge wa vitendo,” aliongeza Husna.
Husna Sungura amesisitiza kwamba anaelewa mahitaji ya wananchi wa Chamanzi kwa sababu yeye ni sehemu ya jamii hiyo. Anajua jinsi wanavyopambana na ukosefu wa huduma za msingi, na anaamini kwamba ana uwezo wa kuleta mabadiliko chanya. Ahadi zake zinajumuisha kuboresha miundombinu, kuimarisha huduma za afya na elimu, na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata fursa ya kiuchumi.
Wananchi wa Chamanzi wameonyesha matumaini yao kwa Husna Sungura, wakiamini kwamba atakuwa mwakilishi wao mwenye uadilifu na kujitolea. Wanasubiri kwa hamu uchaguzi ujao ili waweze kumchagua mtu ambaye ataleta maendeleo yanayolengwa.