Kasigwa Adram Achukua Fomu Kugombea Ubunge Msalala, Aahidi Mabadiliko Makubwa

politics | Thu May 22 2025


Kasigwa Adram Achukua Fomu Kugombea Ubunge Msalala, Aahidi Mabadiliko Makubwa

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kichama Kahama, Kasigwa Adram, leo Mei 22, 2025, amechukua rasmi fomu ya kuwania kiti cha ubunge katika Jimbo la Msalala. Akiwa na matumaini makubwa, ameahidi kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kuondoa mbunge aliyepo madarakani, kupitia vipaumbele vitatu muhimu ambavyo vinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.


Akizungumza baada ya kuchukua fomu katika uzinduzi wa zoezi la uchukuaji wa fomu za ubunge na udiwani ndani ya chama hicho, Kasigwa alieleza kuwa vipaumbele vyake vikuu ni afya, kilimo, elimu ya sayansi na TEHAMA, pamoja na utawala bora.


"Nitahakikisha wananchi wanapata bima za afya ili kupunguza gharama za matibabu, tutapunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, tutaleta ruzuku ya pembejeo za kilimo ili kuongeza uzalishaji, tutahakikisha kuna masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima, na tutasimamia elimu bora ya sayansi na TEHAMA ili kuwaandaa vijana wetu kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Sambamba na hayo, tutadumisha utawala bora kwa maendeleo ya watu wetu," alisema Kasigwa.


Zoezi la uchukuaji wa fomu limezinduliwa leo na linatarajiwa kukamilika Mei 30, 2025. Chama kimeweka wazi kuwa mwanachama yeyote atakayebainika kutoa au kupokea rushwa ili kupitishwa, ataondolewa mara moja kwenye mchakato wa uchaguzi.


Kwa upande wake, Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Kahama, Benedict Shija, alisema kuwa chama kimejipanga kikamilifu kusimamisha wagombea katika asilimia 100 ya nafasi za urais, ubunge, na udiwani nchi nzima.


"Sifa za kugombea ni kuwa na umri wa kuanzia miaka 21 kwa ubunge na udiwani, na miaka 41 kwa nafasi ya urais. Fomu ya udiwani ni Shilingi 30,000, ubunge na viti maalum ni Shilingi 100,000, na fomu ya urais ni Shilingi 1,000,000," alieleza Shija.


Aidha, aliwaonya wanachama dhidi ya kujihusisha na vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa chama hakiwezi kumvumilia mgombea yeyote mwenye tabia ya kutumia pesa au ushawishi haramu kupata nafasi za uongozi. Alisisitiza kuwa chama kinataka wagombea wenye uadilifu na wanaojali maslahi ya wananchi.


Hii ni hatua muhimu katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, na inaonyesha kuwa ACT Wazalendo imejipanga kuleta mabadiliko katika siasa za Tanzania.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.