ACT-Wazalendo Shinyanga Yapokea Watiania Nane Kugombea Ubunge 2025

politics | Wed May 21 2025


ACT-Wazalendo Shinyanga Yapokea Watiania Nane Kugombea Ubunge 2025

Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Shinyanga kimeanzisha rasmi mchakato wa ndani wa kuchukua na kupokea majina ya wanachama wanaotaka kugombea nafasi za ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hadi sasa, watiania nane wamechukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hizo.


Kwa mujibu wa Afisa wa Organizesheni na Mafunzo ya Uchaguzi kutoka ACT-Wazalendo Taifa, Bw. Risasi Semasaba, zoezi hilo lilianza leo, Mei 21, 2025, katika majimbo ya Shinyanga Mjini, Kishapu, Solwa, na jimbo jipya la Itwangi. Majimbo ya Kahama yanatarajiwa kufuata baadae.


Bw. Semasaba alifafanua kuwa hadi sasa, watiania wanane wamejitokeza kuchukua fomu hizo, na zoezi la uchukuaji wa fomu litaendelea hadi Mei 31, 2025. Baada ya hapo, chama kitafanya kura za maoni ili kumpata mgombea mmoja kwa kila jimbo.


“Katika Jimbo la Shinyanga Mjini, waliotia nia ni Siri Yasini, Melkyoli Sebastian, Justa Denis, Simon Tungu, na Mbaruku Haji. Jimbo la Kishapu lina mtiania Yakob Madoshi, Itwangi lina Hassan Ibrahimu, huku Jimbo la Solwa likiwakilishwa na Machanga Machanga,” alisema Bw. Semasaba.


Watania hao wa nafasi za ubunge, akiwemo Bi. Siri Yasini, walieleza mipango yao iwapo watapata ridhaa ya kuwa wabunge. Bi. Yasini alisema kuwa ataanza na vipaumbele vya kuboresha miundombinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na barabara, ujenzi wa masoko, stendi za mabasi, na huduma za afya.


Aliongeza kuwa Shinyanga ni mkoa wenye rasilimali nyingi, ikiwa ni pamoja na madini, na ni mkoa wa tatu kwa kuchangia pato la taifa, lakini bado uko nyuma kimaendeleo. Alisema kuwa akipata ridhaa ya kuwa mbunge, atahakikisha rasilimali hizo zinachangia maendeleo ya mkoa huo.


Mtiania mwingine, Bw. Hassan Ibrahimu kutoka Jimbo la Itwangi, alisema kuwa jimbo hilo ni jipya, na akipata ridhaa ya kuwa mbunge, atahakikisha maendeleo yanapatikana kwa ustawi wa maisha ya wananchi. Aliahidi kuwa atakuwa jimboni muda wote kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.