Joto la kisiasa nchini Tanzania limezidi kupanda baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutoa tamko zito na la kishindo la kutotambua matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, huku kikitaka zoezi hilo lifutwe mara moja. Chama hicho kikuu cha upinzani kimeeleza kuwa mchakato huo haukuwa na chembe ya uhalali, huru, wala haki, na hivyo haupaswi kubarikiwa na Watanzania wapenda demokrasia.
Msimamo huo umewekwa hadharani leo jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), Mheshimiwa John Heche, mara baada ya kumalizika kwa kikao kizito cha Kamati Kuu ya chama hicho. Akizungumza kwa hisia kali na kunukuu maazimio ya kikao hicho, Heche amesema chama chao hakiwezi nharibia macho ukiukwaji mkubwa wa taratibu uliofanyika, akisisitiza kuwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) imeshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo inapaswa kuvunjwa ili kupisha muundo mpya utakaoaminika.
"Hatuwezi kuuma maneno katika hili. Msimamo wa Kamati Kuu ni kwamba tunaunga mkono kilio cha Watanzania na makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yamepaza sauti kukosoa uchaguzi huu. Huu haukuwa uchaguzi, bali ni kiini macho," alisisitiza Heche wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Hoja ya CHADEMA haikujikita kwenye malalamiko ya ndani pekee, bali imepata nguvu mpya kutokana na ripoti za waangalizi wa kimataifa. Heche alibainisha kuwa ripoti kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeweka wazi "madudu" yaliyofanyika. Ripoti hizo zimeainisha kukosekana kwa uwanja sawia wa kisiasa (level playing field), jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wapinzani kwa miaka mingi nchini Tanzania.
"Ripoti za waangalizi wa uchaguzi, zikiwamo zile za SADC, AU na EAC, zimeonesha bila kificho ukosefu wa uwanja sawia na kuhoji uhalali wa mchakato mzima. Mambo yote yaliyoainishwa na wataalamu hawa wa kimataifa yanathibitisha kile ambacho CHADEMA imekuwa ikikipigia kelele siku zote. Hii inatupa nguvu ya kuendelea kudai mabadiliko ya kweli ya kikatiba, kisheria na kitaasisi," aliongeza Heche.
Mwanasiasa huyo machachari alifafanua kuwa lengo la CHADEMA si tu kulalamika, bali kuhakikisha Tanzania inapata mfumo imara ambapo sanduku la kura litaheshimiwa. Alirejea mwito wa muda mrefu wa chama hicho wa kuhitaji Katiba Mpya itakayozaa Tume huru itakayoendesha chaguzi kwa uwazi mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya za kimataifa, bila upendeleo wala shinikizo kutoka kwa dola.
Kauli hii ya CHADEMA inatarajiwa kuibua mjadala mpya katika ulingo wa siasa nchini, ikizingatiwa kuwa suala la Tume Huru ya Uchaguzi limekuwa "mfupa mgumu" katika mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa kwa muda mrefu. Kwa sasa, macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa kwa mamlaka husika kuona ni hatua gani zitachukuliwa kujibu hoja hizi nzito zilizoungwa mkono na ripoti za kidiplomasia.