Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amewataka wakazi wa Kanda ya Ziwa kujiuliza swali gumu kuhusu mustakabali wao, akishangazwa na namna eneo hilo limebaki nyuma kimaendeleo licha ya nchi kutawaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa zaidi ya miongo sita. Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Sengerema, Doyo alieleza kuwa ni aibu kwa Taifa lenye utajiri mkubwa wa rasilimali kama dhahabu, almasi na tanzanite, lakini wananchi wake wanaendelea kuteseka na ukosefu wa huduma muhimu.
"Nchi hii ina kila aina ya madini, lakini ukienda vijijini hakuna maji safi, zahanati hazina dawa, na barabara ni mbovu. Hili halikubaliki na ni ishara ya wazi ya uongozi ulioshindwa," alisisitiza Doyo mbele ya umati wa wananchi.
Akizungumzia kilimo, ambacho ni uti wa mgongo wa wakazi wengi wa Sengerema, mgombea huyo aliahidi kuwakomboa wakulima kutoka kwenye kile alichokiita "mfumo wa unyonyaji." Alisema serikali yake itahakikisha wakulima wanapata masoko huru na yenye bei za ushindani, badala ya kulazimishwa kuuza mazao yao kwa bei za kupangiwa ambazo zinawanufaisha wachache na kuwaacha wao katika lindi la umaskini.
"Sitakubali kuona mkulima anatumia nguvu na gharama kubwa kulima, halafu anakuja mtu kumpangia bei ya hasara. Hizi ni mbinu za kuwadumaza kiuchumi ili muendelee kuwa wategemezi. Tutaondoa utaratibu huu na kuhakikisha jasho lenu linalipa," aliahidi Doyo.
Aidha, aligusia kero za wasafirishaji, akisema madereva na wamiliki wa vyombo vya moto wanashindwa kupata faida kutokana na gharama kubwa za matengenezo zinazosababishwa na ubovu wa barabara. Alisema ni unafiki kwa serikali kudai kodi kubwa kutoka kwa wafanyabiashara hao huku ikishindwa kuwekeza kwenye miundombinu inayorahisisha shughuli zao za kiuchumi.
Doyo alihitimisha kwa kusema kuwa CCM imekuwa ikirudia ahadi zilezile kila kipindi cha uchaguzi bila kuzitekeleza, na sasa ni wakati wa wananchi wa Kanda ya Ziwa kufanya maamuzi sahihi ifikapo Oktoba 29. Baada ya mkutano huo, msafara wake uliendelea na safari kuelekea wilayani Ngara, mkoani Kagera.