Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameelezea masikitiko yake makubwa juu ya hali duni inayoendelea kuwakabili wakulima wa korosho katika mikoa ya kusini mwa Tanzania, licha ya zao hilo kuwa na thamani kubwa kimataifa. Akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Liwale mkoani Lindi, Mwalimu alifananisha korosho na "dhahabu ya Kusini," akisema ni jambo la kusikitisha kuona wanaolima dhahabu hiyo wakiendelea kuogelea kwenye dimbwi la umaskini.
Alisema tatizo kubwa linalowakwamisha wakulima ni mfumo wa sasa unaowanufaisha zaidi watu wa kati na madalali, ambao hununua korosho kwa bei ndogo na kwenda kuziuza kwa faida kubwa, huku mkulima akibaki na hasara. "Jasho la mkulima wa korosho linawatajirisha walanguzi badala ya kumnufaisha yeye mwenyewe. Hali hii lazima ifike mwisho. Serikali ya CHAUMMA itahakikisha inabadili mfumo huu na kumweka mkulima kwanza," alisisitiza Mwalimu mbele ya umati.
Katika hatua isiyo ya kawaida, aliwasihi wakulima wasikimbilie kuuza korosho zao za msimu huu, akiahidi kuwa serikali yake itakapongia madarakani itaweka bei elekezi itakayokuwa na tija na kulinda maslahi yao. Alieleza kuwa mpango wake mkuu ni kusitisha uuzaji wa korosho ghafi nje ya nchi na badala yake kujenga viwanda vya usindikaji katika kila mkoa unaolima zao hilo. "Hakuna maana kuuza mali ghafi kwa bei chee wakati tuna uwezo wa kuibangua na kuisindika hapa nchini. Tukifanya hivyo, tutauza bidhaa iliyoongezewa thamani kwa bei ya juu hata mara tano zaidi na kumuinua mkulima wetu," alieleza.
Zaidi ya hayo, Mwalimu aliahidi kuwa serikali yake itaboresha miundombinu ya vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao, na pia itaanzisha mfumo wa kuwapatia wakulima mikopo yenye masharti nafuu pamoja na pembejeo za kisasa ili waweze kuongeza uzalishaji na ufanisi katika mashamba yao.