Katika kile kinachoonekana kama 'pumzi mpya' na faraja kubwa kwa Watanzania wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU), Serikali imetoa kauli nzito na ya kishujaa ikihakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayeteseka kwa kukosa dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo (ARVs). Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi, ameweka bayana kuwa ghala la taifa limesheheni dawa hizo kwa asilimia 100 na zinatolewa bure kabisa, bila chenga wala urasimu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi na tamko rasmi la maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka 2025, Waziri Lukuvi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha afya ya kila Mtanzania inalindwa kwa wivu mkubwa. Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu inayochagiza vitendo zaidi: “Imarisha Mwitikio, Tokomeza UKIMWI”.
Upatikanaji wa Dawa na Mwitikio wa Wananchi Waziri Lukuvi, kwa takwimu zisizo na mashaka, amebainisha kuwa mwamko wa wananchi kutumia dawa za ARV umekua kwa kasi ya kuridhisha. Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha WAVIU wanaotumia dawa hizo kimepanda kutoka asilimia 98 mwaka 2024 hadi kufikia asilimia 98.5 mwaka 2025. Hii ni ishara njema kwamba elimu imepenya hadi vijijini na unyanyapaa unaendelea kupungua, jambo linalochochea watu kujitokeza kupata huduma bila kificho.
"Ndugu zangu, dawa zipo za kumwaga na ni bure. Serikali imehakikisha mnyororo wa ugavi wa dawa hizi hauyumbi ili kulinda afya za wananchi wetu. Ongezeko hili la matumizi ya dawa ni ushahidi tosha kuwa Watanzania wameelewa umuhimu wa kufubaza virusi ili kuendelea na ujenzi wa taifa," alisisitiza Lukuvi.
Kusogeza Huduma 'Mlangoni' Katika kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anayetembea umbali mrefu kufuata "dozi", serikali imepanua wigo wa miundombinu ya afya. Waziri Lukuvi ametangaza ongezeko kubwa la vituo vya kutolea huduma za tiba na matunzo (Care and Treatment Centers - CTCs). Vituo hivyo vimeongezeka kutoka 7,805 mwaka 2024 hadi kufikia vituo 8,203 mwaka 2025. Hatua hii ni mapinduzi makubwa katika sekta ya afya, ikilenga kumfikishia mwananchi huduma bora popote alipo.
Teknolojia ya Maabara Yaboreshwa Vita dhidi ya UKIMWI si dawa tu, bali pia vipimo sahihi vya mara kwa mara. Katika eneo hili, Waziri Lukuvi ameeleza kuwa serikali imefanya uwekezaji wa maana kwenye vifaa tiba. Idadi ya mashine za kisasa za kupima wingi wa virusi mwilini (Viral Load Machines) imeongezeka na kufikia jumla ya mashine 177 zinazochapa kazi nchi nzima. Kati ya hizo, mashine kubwa zimeongezeka kutoka 43 hadi 50, huku mashine ndogo zikiwa 127.
Hii inamaanisha kuwa majibu ya vipimo sasa yanapatikana kwa haraka zaidi, kumuwezesha daktari na mgonjwa kujua maendeleo ya afya na ufanisi wa dawa anazotumia.
Wito kwa Jamii na Kukumbuka Mashujaa Akiitimisha tamko hilo, Waziri Lukuvi amesisitiza kuwa Siku ya UKIMWI Duniani si siku ya sherehe, bali ni siku ya tafakuri jadidi. Ni wakati wa kupima tulipotoka, tulipo, na tunapoelekea katika vita hii. Amewataka Watanzania kutumia siku hii kuwakumbuka ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huu, na kuwajali yatima walioachwa.
"Mapambano haya yanahitaji umoja wetu sote. Serikali inaweka sera na miundombinu, lakini jamii ndiyo yenye jukumu la kuzuia maambukizi mapya na kuwapenda wanaoishi na VVU. Tuendelee kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha ajenda hii inabaki kuwa kipaumbele," alihitimisha Mhe. Lukuvi.