Shirika la Afya Duniani (WHO) limezitaka nchi wanachama na wadau wa afya duniani kuongeza ufadhili wa programu za afya ili kunusuru wagonjwa, hasa wale wanaotegemea dawa za kufubaza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (ARVs).
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, akizungumza Machi 18, 2025, mjini Geneva, Uswisi, alieleza kuwa nchi 50 tayari zimeathirika na ukosefu wa rasilimali za afya, huku nchi nane zikitarajiwa kuishiwa kabisa na dawa za ARVs ndani ya miezi mitatu ijayo.
Athari kwa Mapambano Dhidi ya VVU na Magonjwa Mengine
Tedros alionya kuwa upungufu wa dawa hizo utarudisha nyuma juhudi za zaidi ya miaka 20 katika mapambano dhidi ya VVU na magonjwa mengine makubwa kama malaria. Alisema hali hii inaweza kuongeza maambukizi ya VVU kwa zaidi ya watu milioni 10.
“Kukosekana kwa misaada kutasababisha athari kubwa, kwani bila vifaa vya kupimia na dawa za kutosha, vifo vitafikia milioni tatu – mara tatu zaidi ya idadi ya vifo vya mwaka jana,” alisema Tedros.
Uamuzi wa Marekani Kuondoa Misaada waathiri WHO
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa uamuzi wa Marekani kusitisha baadhi ya misaada yake kwa WHO umechangia changamoto hiyo, na athari zake zitakuwa kubwa kwa nchi zinazoendelea.
“Marekani inapaswa kutathmini uamuzi wake kwa heshima ya ubinadamu, kwani hatua hii si tu itaathiri mataifa mengine bali pia inaweza kuhatarisha afya ya dunia nzima,” aliongeza Tedros.
WHO inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha dawa na vifaa vya matibabu vinapatikana kwa wagonjwa, huku ikihimiza ushirikiano wa dharura katika kufanikisha juhudi hizo.