'Amri Yako ni Kituko!' - Mnyika Amchana Jaji Mwanga, Awasilisha Malalamiko Tume ya Maadili

politics | Tue Jul 15 2025


'Amri Yako ni Kituko!' - Mnyika Amchana Jaji Mwanga, Awasilisha Malalamiko Tume ya Maadili

Katika hali isiyo ya kawaida mahakamani, Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amesimama mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Hamidu Mwanga, na kumweleza waziwazi kuwa amri alizozitoa dhidi ya chama hicho ni za "kuchekesha" au kwa lugha nyingine "kituko," na hivyo kumtaka ajiondoe katika kusikiliza kesi yao kwa madai ya kutotenda haki.


Mvutano huo mkali ulitokea jana katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo Mnyika, kwa niaba ya chama na Bodi ya Wadhamini, aliwasilisha hoja za kumtaka Jaji Mwanga ajiondoe, akidai ana maslahi na kesi hiyo na anatumika kukihujumu chama hicho.


Mnyika alidai kuwa Jaji Mwanga amekiuka misingi ya utoaji haki katika matukio kadhaa. Miongoni mwa malalamiko makuu ni kitendo cha Jaji huyo anayedaiwa kukataa kuahirisha kesi Juni 10, 2025, ili kutoa fursa kwa mawakili wa CHADEMA, Jebra Kambole na Hekima Mwasipu, kwenda kwenye msiba wa ajali mbaya iliyotokea Mbeya. "Ulitunyima haki ya uwakilishi unaostahili kwa sababu ya msiba, kitendo kilichomlazimu Wakili Kambole kujiondoa," alidai Mnyika.


Pili, Mnyika alidai Jaji Mwanga alionesha upendeleo aliposhughulikia suala la notisi ya mmoja wa waleta maombi, Maulida Anna Komu, kutaka kujitoa kwenye kesi. Alidai kuwa Jaji aliamua kuwa notisi hiyo imeghushiwa na akaamuru wakili aliyeiwasilisha (Edson Kiratu) akamatwe na polisi bila kumpa fursa ya kujieleza, kitendo alichokiita ukiukwaji mkubwa wa haki ya kusikilizwa.


"Ulifanya uamuzi bila kuzingatia misingi ya haki dhidi ya Wakili Kiratu na dhidi ya suala zima la notisi ya kujitoa kwa mama Komu. Tunaona hukutenda haki," alisisitiza Mnyika.


Katika shambulio la moja kwa moja, Mnyika alimwambia Jaji Mwanga kuwa amri yake ya kukizuia CHADEMA kufanya siasa na ile inayohusu mali za chama, zinalenga kukiharibu chama. "Kazi ya chama cha siasa ni kufanya siasa; ukikizuia ni umekiua. Hizo amri ulizotoa ni za kuchekesha, ni kituko," alisema Mnyika.


Aidha, alieleza kuwa tayari wamewasilisha malalamiko rasmi dhidi ya Jaji Mwanga kwenye Tume ya Maadili ya Majaji, wakidai kuwa historia yake ya kuwa Mkurugenzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inamfanya awe na mgongano wa maslahi.


Baada ya kusikiliza hoja hizo nzito kutoka kwa pande zote, Jaji Mwanga aliahirisha kesi hiyo na kusema atatoa uamuzi wa kujiondoa au kutoondoka kwenye kesi hiyo Julai 28, 2025.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.