Zuio la Kisiasa CHADEMA: Waliotajwa Hawaruhusiwi Hata Kuzungumza na Vyombo vya Habari!

politics | Thu Jul 17 2025


Zuio la Kisiasa CHADEMA: Waliotajwa Hawaruhusiwi Hata Kuzungumza na Vyombo vya Habari!

Wakili Shabaan Marijani amesisitiza kuwa watu wote waliotajwa katika zuio la Mahakama Kuu la kutokushiriki shughuli zozote za kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hawaruhusiwi hata kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala yanayohusu chama hicho. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Wakili Marijani alifafanua juu ya ufafanuzi wa kisheria uliotolewa kufuatia zuio lililotoka Juni 10, 2025, lililotolewa na Jaji Hamidu Mwanga, na kusisitiza kuwa kukiuka amri hiyo ni dharau kwa Mahakama.


Zuio hili linatokana na shauri dogo namba 8960/2025 katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam. Wakili Marijani alieleza bayana kuwa, iwapo watu hao watahitaji kuzungumza na vyombo vya habari, wanapaswa kueleza mambo mengine ambayo hayaingiliani na amri ya zuio hilo. "Hawatakiwi hata kuzungumza na waandishi wa habari kwa sababu tayari Mahakama ilishatoa amri ya zuio; hapo wanakuwa wamekiuka amri hiyo," alifafanua Wakili Marijani.


Kwa upande wake, Wakili Gizo Simfukwe alieleza kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu wahusika 10 wa zuio hilo kutokana na baadhi ya watu kujaribu kujitenga na kudai hawahusiki. Aliongeza kuwa, kutokana na upotoshaji uliokuwa ukiendelea, wao kama wanasheria wanaowawakilisha wateja waliofungua kesi hiyo waliandika barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, wakiomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu nani hasa anahusika na zuio hilo.


Wakili Simfukwe alithibitisha kuwa wamepokea barua ya majibu kutoka kwa Msajili wa Mahakama, iliyoandikwa Julai 14, 2025. Nakala ya barua hiyo pia imetumwa kwa upande wa pili wa kesi hiyo. Msajili amesisitiza kuwa zuio hilo linawahusu watu wote waliotajwa, na litaendelea hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.


Watu waliotajwa na zuio hilo ni pamoja na Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara au Kaimu Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Zanzibar au Kaimu Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Zanzibar, Katibu Mkuu wa CHADEMA au Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara au Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Zanzibar au Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Zanzibar.


Aidha, zuio hili linawahusu viongozi wote na katika ngazi zote, iwe ni viongozi walioteuliwa moja kwa moja katika nafasi zao za uongozi au wanaokaimu katika nafasi zao. Pia linawahusu mfanyakazi yeyote au wakala au mtu yeyote yule anayefanya kazi hizo kwa niaba ya CHADEMA, au aliyepewa maelekezo au kuiwakilisha CHADEMA, atakayefanya kazi zozote za kisiasa kwa kutokea Taifa, Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa, na maeneo yote nchini kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bara na Zanzibar.


Wakili Simfukwe alionya kuwa mtu yeyote atakayekwenda kinyume na uamuzi wa Mahakama atakuwa anatenda kosa la jinai la kudharau amri ya Mahakama, na anaweza kuchukuliwa hatua zingine za kimadai kwa mujibu wa sheria. "Mahakama inapoelekeza na wewe ukaenda kinyume na Mahakama kwa kujificha kwenye mwavuli kwamba mimi hainihusu, huo utakuwa ni uvunjaji wa sheria. Tumeamua kutoa ufafanuzi huu kwa umma kuondoa upotoshaji kwa baadhi ya watu," alimalizia Wakili Simfukwe.


Zuio hili lilitolewa kufuatia kesi ya madai namba 8960/2025 iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu. Mahakama ilikubali maombi hayo na zuio lilitolewa kwa mujibu wa amri ya Jaji Hamidu Mwanga katika shauri dogo la madai namba 8960 la mwaka 2025, wakati uamuzi wa maombi katika kesi kuu ya madai namba 8323/2025 ulipotoa zuio hilo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.