Katika kongamano la nne la Operesheni Linda Demokrasia lililofanyika mkoani Songwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, ametoa ujumbe mzito kwa serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), akisisitiza kuwa chama chake kiko tayari kuongoza harakati za kweli za kidemokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Semu, akihutubia wanachama na wapenzi wa chama kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine, amewapongeza kwa kujitolea na kusimama imara katika kulinda demokrasia. Alisema kuwa kongamano hilo si mkutano wa kawaida, bali ni wito wa kihistoria kwa Watanzania wote kuamka na kupigania haki, usawa, na uhuru wa kweli.
Ameeleza kuwa kongamano hilo limejengwa juu ya misingi ya mikutano mingine mitatu iliyofanyika Dar es Salaam, Lindi, na Kigoma, na inaonyesha nia ya chama hicho kujenga mfumo wa haki katika siasa za Tanzania. Semu amefafanua kuwa Operesheni Linda Demokrasia ni zaidi ya kampeni ya kisiasa, bali ni harakati za ukombozi wa kisiasa nchini.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, Semu amelaani vikali vitendo vya uvunjifu wa haki na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wapinzani. Alitoa mfano wa kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Songwe, Ndugu Zambi, na kushambuliwa kwa Katibu wa Mkoa, Ndugu Kelvin, akisema matukio hayo yanaonyesha jinsi chama tawala kilivyopoteza dira ya haki. "Je, CCM inaweza kweli kujivunia ushindi unaotokana na mateso ya wananchi?" alihoji Semu. "Hii sio demokrasia – ni udikteta uliovaa suti ya uchaguzi."
Semu amesisitiza kuwa chama chake hakitakubali hofu kuwa silaha ya kuwavunja moyo Watanzania. Alieleza kuwa ACT Wazalendo iko tayari kuongoza "uasi wa haki" dhidi ya mifumo ya ukandamizaji, huku akimpongeza Tundu Lissu wa CHADEMA kwa kusimama imara licha ya changamoto za kisiasa. "Mashtaka dhidi ya Lissu hayatuzuii – yanatupa nguvu zaidi ya kuendelea! Niko tayari kuongoza mapambano haya kwa niaba ya Watanzania wote," alisema kwa msisitizo.
Semu ameweka wazi madai sita ya msingi ambayo ACT Wazalendo inapigania kupitia Operesheni Linda Demokrasia. Madai hayo ni pamoja na:
1. Makamishna wa Tume ya Uchaguzi wajiuzulu na wateuliwe upya kwa mujibu wa sheria.
2. Mawakala wa vyama wawe huru na wapate fomu za matokeo bila kizuizi.
3. Wagombea wasienguliwe bila sababu za msingi.
4. Kudhibiti kura feki.
5. Wakurugenzi wa Halmashauri wasihusike kama wasimamizi wa uchaguzi.
6. Vyombo vya ulinzi visitumike kuvuruga uchaguzi.
Akitilia mkazo madai hayo, Semu amesema sio magumu. "Madai haya sio magumu – yanahitaji tu uamuzi wa kisiasa. CCM wanajua kuwa wakishindana kwa usawa, hawana nafasi ya kushinda," amesema. Hotuba yake inaashiria kuwa ACT wazalendo wamejipanga kikamilifu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.