ACT Wazalendo Yatangaza Sababu Kuu Tatu za Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Yawaahidi Wananchi Mapambano ya Kutetea Demokrasia

politics | Wed Apr 16 2025


ACT Wazalendo Yatangaza Sababu Kuu Tatu za Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Yawaahidi Wananchi Mapambano ya Kutetea Demokrasia

Chama cha ACT Wazalendo kimeweka wazi sababu tatu muhimu zinazowasukuma kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025, ambazo ni pamoja na kutetea na kulinda thamani ya kura za wananchi. Chama hicho kimeeleza kuwa kina wasiwasi mkubwa kuhusu kupotea kwa thamani ya kura, kutokana na uzoefu wa uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, Uchaguzi Mkuu 2020, na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.


Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni katika ofisi za chama hicho Vuga, Zanzibar, Kiongozi wa Chama, Bi. Dorothy Semu, alisema kuwa viongozi hawachaguliwi tena kwa kura za wananchi, bali kwa nguvu ya dola. Alisema hali hii ni mapinduzi dhidi ya haki ya raia ya kuchagua viongozi wao, haki ambayo ndiyo inathibitisha uraia wao, na kwamba hujuma hii haikubaliki.


Bi. Semu alisisitiza kuwa ACT Wazalendo inatambua kuwa uchaguzi si mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi wenyewe. Kwa kutambua dhima kubwa iliyopo, chama hicho kinakusudia kuhamasisha vuguvugu kubwa la wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu 2025 ili kutetea na kulinda haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.


"ACT Wazalendo tutautumia Uchaguzi Mkuu 2025 kama jukwaa la kuitetea na kuilinda demokrasia yetu. Ni vizuri niseme hapa kuwa tumejiandaa kwa hili. CCM ijue kuwa tutaikabili vile itakavyokuja. Tupo tayari kuwaongoza Watanzania kupitia vuguvugu la wananchi kutetea thamani ya kura ili kulinda msingi wa katiba yetu kuwa madaraka yote yanatoka kwa wananchi. Tupo tayari kwa mapambano!" alisisitiza Bi. Semu.


Aidha, alieleza kuwa kususia uchaguzi kunaweza kuimarisha hujuma dhidi ya demokrasia. Baada ya kufanya tathmini ya kina, chama kimejiridhisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kitafurahia iwapo vyama makini vya upinzani vitasusia uchaguzi, ili kiendeleze hujuma zake dhidi ya demokrasia nchini.


Bi. Semu alisema ACT Wazalendo imekataa kuwapa fursa hiyo CCM, kwa sababu uchambuzi wao unaonyesha kuwa katika nchi mbalimbali duniani, kususia uchaguzi kumeimarisha hujuma za dola dhidi ya demokrasia, kwa kutoa mwanya wa kupora kwa urahisi sauti ya wananchi. Alitoa mifano ya Kenya (2017), Misri (2018), Ivory Coast (2020), Zanzibar (2015), na Venezuela (2018).


Alisisitiza kuwa ACT Wazalendo itaenda kutumia Uchaguzi Mkuu 2025 kama uwanja wa mapambano ya kuzuia hujuma dhidi ya demokrasia na kudai mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi. Kwao, Uchaguzi Mkuu 2025 ni uwanja wa mapambano.


Pia, alieleza kuwa wanashiriki uchaguzi ili kutoa jukwaa kwa vijana wasio na ajira, wakulima na wafanyakazi wanaonyonywa, wananchi waliokandamizwa, kupuuzwa na kuonewa, na kupigania taifa la wote, maslahi ya wote.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.