Katika kile kinachoonekana kama kumpunguzia mzigo mfanyakazi wa ofisini na kuongeza ufanisi wa kazi, kampuni ya Google imetangaza mapinduzi makubwa yanayolenga kubadilisha jinsi tunavyofanya kazi maofisini. Siku ya Jumanne, tarehe 3 Desemba, Google ilizindua jukwaa jipya liitwalo ‘Google Workspace Studio’. Hili ni 'kivuko' kipya kinachomwezesha mfanyakazi yeyote—awe mhasibu, afisa rasilimali watu, au meneja masoko—kutengeneza "Wakala wa AI" (AI Agent) wake mwenyewe wa kumfanyia kazi, bila kuhitaji kuwa na ujuzi wa IT au kuandika kodi za kompyuta.
Hatua hii ni jibu la moja kwa moja la Google dhidi ya mshindani wake mkubwa, Microsoft, ambaye amekuwa akitamba na mfumo wake wa Copilot maofisini, na pia ni changamoto kwa OpenAI (ChatGPT) ambayo imekuwa ikijaribu kuingia kwenye soko la makampuni.
Mkombozi wa "Wazee wa Kazi za Kujirudia"
Shida kubwa ambayo makampuni yamekuwa yakikumbana nayo ni kwamba, mara nyingi wataalamu wa IT hutengeneza mifumo migumu ambayo wafanyakazi wa kawaida wanashindwa kuitumia. Google wameiona fursa hapo.
Farhaz Karmali, Mkurugenzi wa Bidhaa wa Google Workspace, amefafanua kwa lugha nyepesi: "Mifumo ya zamani ilikuwa migumu sana kwa mtu wa kawaida. Sasa tunataka kila mtu awe na uwezo wa kuunda roboti yake ya kumsaidia kazi za kuchosha."
Kwa kutumia nguvu ya mfumo mpya wa ‘Gemini 3’, Workspace Studio inakuruhusu kutoa maelekezo kwa maneno ya kawaida (prompts) au kuchagua templeti zilizotengenezwa tayari. Kwa mfano, unaweza kuunda roboti itakayofanya yafuatayo:
- "Faili likiingia kwenye folda hii ya Google Drive, tengeneza ripoti na unitumie."
- "Barua pepe ikitoka kwa bosi yenye neno 'Haraka', ibadilishe kuwa tiketi ya kazi kwenye mfumo wa Jira au Salesforce."
- Kupanga ratiba za vikao na kuwajibu wateja kiotomatiki kwa lugha ya kiofisi.
Urahisi wa Maisha: Kila Kitu Ndani ya Gmail na Docs
Uzuri wa mfumo huu ni kwamba unafanya kazi ndani ya programu ambazo Watanzania wengi wamezizoea—Gmail, Google Docs, Sheets, na Drive. Hakuna haja ya kufungua programu mpya na kuanza kujifunza upya. Roboti wako atakaa pembeni mwa skrini (Side Panel) akikupa ripoti ya nini kimefanyika na nini kinasubiriwa.
Hii ni habari njema kwa wafanyakazi wa maofisi hapa nchini ambao hutumia muda mwingi kufanya kazi za "copy and paste" au kujibu barua pepe zinazofanana kila siku. Sasa, unaweza kumwachia roboti amalize hayo huku wewe ukifanya kazi za msingi zaidi.
Vita ya Masoko: Google vs Microsoft
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanasema Google ina faida kubwa moja: "Data za Nyumbani." Tofauti na mifumo mingine inayojaribu kujifunza kutoka nje, Google tayari inazo data zako (kwa usalama) kupitia barua pepe na nyaraka unazohifadhi kila siku. Hii inamfanya roboti wa Google awe na "akili" zaidi ya kuelewa muktadha wa kazi yako kuliko roboti mwingine yeyote.
Wakati Microsoft akiwa amewekeza sana kwenye Office 365 Copilot na Amazon (AWS) akija na QuickSight, Google imeamua kucheza karata yake kwenye urahisi wa matumizi kwa mtu wa kawaida asiye na ujuzi wa kiufundi.
Kwa wafanyabiashara na mashirika ya Tanzania, huu ni wakati wa kuanza kufikiria jinsi ya kutumia zana hizi kuongeza tija. Badala ya kuajiri mtu maalum wa kupanga faili, sasa unaweza "kumwajiri" roboti wa Google Workspace Studio akufanyie kazi hiyo bure au kwa gharama nafuu ya kifurushi chako cha ofisi.