Katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali ambapo taarifa binafsi zimekuwa bidhaa adimu kama pembe za ndovu, kumezuka taharuki kubwa miongoni mwa watumiaji wa mtandao duniani na hapa Tanzania. "Ubuyu" uliosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii ulidai kuwa kampuni ya Google inatumia barua pepe (Emails) zetu za siri na nyaraka zilizoambatishwa (attachments) ndani ya 'Gmail' ili kuifundisha Akili Mnemba yake inayojulikana kama 'Gemini'.
Madai hayo yalizua hofu kuwa siri za watu, kuanzia mikataba ya biashara hadi maongezi ya kifamilia, zinatumiwa bila ridhaa kukuza uwezo wa roboti huyo. Hata hivyo, Google imeibuka na kukanusha vikali madai hayo, ikisisitiza kuwa faragha ya mtumiaji ni kipaumbele chao namba moja.
Google Yatoa Ufafanuzi wa Kina
Akizungumza katika mahojiano na mtandao wa teknolojia wa The Verge, Msemaji wa Google, Bi. Jenny Thompson, amewatoa hofu watumiaji akisema kuwa taarifa zinazosambaa ni upotoshaji mtupu.
"Baadhi ya ripoti zinapotosha umma," alisema Thompson. "Google haijawahi kubadilisha mipangilio (settings) ya watumiaji kwa siri. Vipengele vya 'Smart Features' vimekuwepo kwa miaka mingi sasa ili kurahisisha matumizi, na tunapenda kuweka wazi kuwa hatutumii maudhui ya Gmail ya watumiaji kufundisha mfumo wetu wa Gemini AI."
Chanzo cha Mkanganyiko
Kiini cha mgogoro huu ni mkanganyiko kuhusu nini maana ya "Smart Features & Personalization" (Vipengele Mahiri na Kubinafsisha) ndani ya Gmail. Google inaeleza kuwa vipengele hivi ndivyo vinavyokuwezesha:
- Kurekebisha Mwandiko: Kusaidia kusahihisha makosa ya sarufi au "spelingi" (Spell check).
- Uchujaji wa Barua Pepe: Kutenganisha barua pepe muhimu na matangazo (Promotions/Social).
- Otomatiki: Kuongeza tiketi za ndege au oda za mizigo moja kwa moja kwenye Kalenda yako ukipokea barua pepe ya uthibitisho.
Google inasema kuchambua barua pepe ili kukupa huduma hizi binafsi ni tofauti kabisa na kuchukua data hizo na kuzipeleka "shule" kufundisha Gemini jinsi ya kuandika au kuongea kwa ajili ya matumizi ya dunia nzima.
Watumiaji Waendelea Kuwa na Mashaka
Licha ya utetezi huo, bado kuna wingu la wasiwasi. Baadhi ya wadau wa teknolojia na watumiaji wa mtandao wamelalamika kuwa walizima (OFF) vipengele hivyo vya 'Smart Features', lakini waliporudi kukagua, walikuta vimewashwa (ON) tena bila ridhaa yao.
Hii inahushishwa na sasisho (update) kubwa lililofanywa na Google mwezi Januari mwaka huu, lililolenga kuunganisha mipangilio ya 'Google Workspace', ramani (Maps), na pochi ya kidijitali (Wallet). Inawezekana kuwa wakati wa maboresho hayo, mipangilio ya baadhi ya watumiaji ilirudi kwenye hali ya awali (default settings), jambo ambalo limezua taharuki kuwa huenda kuna mchezo mchafu unaendelea chini kwa chini.
Angalizo kwa Watanzania
Suala hili ni kengele ya hatari kwa watumiaji wa mitandao nchini Tanzania. Kadiri tunavyozidi kutegemea teknolojia—kuanzia wanafunzi wa vyuo vikuu hadi wafanyabiashara wa Kariakoo—ni muhimu kuelewa jinsi data zetu zinavyotumika.
Ingawa Google inasema kwenye sera zake kuwa "Tunatumia maudhui na shughuli zako kubinafsisha uzoefu wako," wanasisitiza kuwa hii ni kwa ajili ya kukusaidia wewe mtumiaji husika, na si kuuza siri zako au kumlisha roboti wa Gemini.
Kama wahenga wasemavyo, "Kinga ni bora kuliko tiba." Google imeshauri watumiaji wote kuchukua muda kuingia kwenye mipangilio yao ya Gmail (Settings) na kukagua sehemu ya 'Smart features and personalization' ili kujiridhisha kama wameridhia au la. Hii itasaidia kuondoa mashaka na kuhakikisha unadhibiti taarifa zako mwenyewe.
Kwa sasa, Google imesimama kidete: Barua pepe zako ni siri yako, na Gemini haihusiki nazo. Lakini katika ulimwengu huu wa AI unaokua kwa kasi, mjadala huu wa faragha unaonekana ndio kwanza unaanza.