Google Yaleta Mapinduzi: 'CC', Karani wa AI Atakayekupangia Ratiba Yako Kila Asubuhi Kabla Hujanywa Chai

it | Thu Dec 18 2025


Google Yaleta Mapinduzi: 'CC', Karani wa AI Atakayekupangia Ratiba Yako Kila Asubuhi Kabla Hujanywa Chai

Hebu vuta picha: Umeamka asubuhi jijini Dar es Salaam, sauti za daladala na bodaboda zimeshaanza kushika kasi. Kabla hata hujapiga mswaki au kunywa chai yako ya rangi, unashika simu yako na kukuta mamia ya barua pepe (emails), mialiko ya vikao, na faili ulizotumiwa usiku wa manane. Unahisi kuchanganyikiwa kabla siku haijaanza.


Hapa ndipo Google wameamua kuingilia kati. Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia duniani imezindua "silaha" mpya ya kukurahisishia maisha kupitia kitengo chao cha majaribio, Google Labs. Mfumo huu mpya wa Akili Mnemba (AI Agent) unaitwa 'CC'.


CC ni Nani Hasa?


Fikiria CC kama Katibu Muhtasi (Secretary) wako binafsi ambaye halali wala haendi likizo. Akitumia ubongo wa mfumo wa Gemini, CC ana uwezo wa kuingia kwenye akaunti yako ya Gmail, Google Drive, na Google Calendar, kisha kuchuja taarifa zote muhimu na kukuandalia ripoti fupi kila asubuhi.


Ripoti hiyo, inayoitwa "Your Day Ahead" (Siku Yako Mbele), inakuja kama barua pepe ya kwanza unayosoma asubuhi. Sio tu inakuonyesha ratiba, bali inachambua na kukuambia: "Leo una kikao na bosi saa nne, na usisahau kuna bili ya maji ilitumwa jana inatakiwa kulipwa."


Tofauti na mifumo ya zamani, CC ana akili ya ziada. Anaweza kukutafutia nyaraka (documents) utakazohitaji kwenye kikao hicho na hata kukuandalia rasimu (draft) ya majibu ya barua pepe ambazo ni za haraka. Ni kama kuwa na msaidizi anayekunong'oneza sikioni, "Mzee, usisahau hili na lile."


Mawasiliano ya Njia Mbili: Sio Kasuku, ni Mshauri


Uzuri wa CC ni kwamba hasemi tu na kuondoka. Unaweza kumjibu (reply) kama unavyomjibu binadamu. Unaweza kumwambia, "CC, tafadhali ongeza kikao na Mama Ntilie saa saba mchana kwenye kalenda," au "CC, nikumbushe kusoma ripoti ya mauzo nikirudi nyumbani."


Kadiri unavyozidi kuwasiliana naye, ndivyo anavyozidi kukuelewa. Anajifunza tabia zako, vipaumbele vyako, na hata mtindo wako wa kufanya kazi. Lengo ni kufanya uzalishaji wako uwe wa juu (productivity maximization) bila kutumia nguvu kubwa.


Vita ya Vigogo: Google vs OpenAI


Hatua hii ya Google inatafsiriwa na wataalamu kama jibu la kibabe kwa mpinzani wao mkubwa, OpenAI. Ikumbukwe mwezi Septemba, OpenAI ilizindua mfumo unaofanana na huu uitwao ‘ChatGPT Pulse’. Bosi wa OpenAI, Sam Altman, aliwahi kusema Pulse ni "kipengele anachokipenda zaidi."


Lakini Google ina turufu moja kubwa ambayo OpenAI haina: Data zako. Google tayari inamiliki barua pepe zako (Gmail), ratiba zako (Calendar), na faili zako (Drive). Kwa kuunganisha vitu hivi vitatu pamoja chini ya 'CC', wanatengeneza mfumo ambao ni "chanda na pete" na maisha yako ya kila siku.


Pia, kumeibuka wimbi la 'Startups' nyingine kama Read AI, Fireflies, na programu ya sauti ya Huxe (iliyotengenezwa na waliokuwa wafanyakazi wa Google) zinazojaribu kufanya kazi hii ya uratibu. Hata Meta (wamiliki wa Facebook na Instagram) wanapika kitu kinaitwa ‘Project Luna’. Hata hivyo, wataalamu wanasema Google ina nafasi kubwa ya kushinda vita hii kwa sababu "imemshika mtumiaji pabaya"—kwenye Inbox ya barua pepe.


Upatikanaji na Masharti


Kwa sasa, huduma hii ya 'CC' inapatikana kwa majaribio (Early Access) nchini Marekani na Canada pekee, na ni kwa watumiaji wenye umri zaidi ya miaka 18 ambao wamelipia vifurushi vya AI Premium (Pro & Ultra). Akaunti za kiofisi (Google Workspace) bado hazijahusishwa, ni kwa ajili ya akaunti binafsi tu kwa sasa.


Ingawa bado haijafika Tanzania rasmi, historia inaonyesha kuwa Google huwa haichelewi kusambaza teknolojia hizi duniani kote pindi majaribio yanapokamilika.


Neno la Mhariri


Kuzinduliwa kwa CC ni ishara tosha kuwa zama za kutumia daftari na kalamu kupanga ratiba zinaelekea ukingoni. Google inataka kuhakikisha kuwa jambo la kwanza unalofanya ukiamka asubuhi ni kuongea na AI wao. Kwa Mtanzania mjasiriamali au mfanyakazi, hii inaweza kuwa mbadala wa kuajiri msaidizi wa ofisi, ikipunguza gharama na kuongeza ufanisi. Swali linabaki, je, tuko tayari kukabidhi maisha yetu yote yapangwe na mashine?

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.