Shirika la ndege la Air India limeingia kwenye kashfa nyingine baada ya hadi watu saba, wakiwemo abiria na wafanyakazi, kudaiwa kupata dalili za sumu ya chakula wakiwa safarini. Tukio hili limetokea huku kukiwa na juhudi za shirika hilo kuboresha huduma zake kufuatia ajali mbaya iliyotokea mapema mwezi huu.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa, ikiwemo Hindustan Times (HT), tukio hilo lilitokea mnamo Juni 24, kwenye ndege ya Air India AI-130 iliyokuwa ikisafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Heathrow jijini London, Uingereza, kuelekea Mumbai, India. Abiria watano na wafanyakazi wawili walilalamika kusikia kichefuchefu na kizunguzungu wakiwa angani.
Katika taarifa rasmi, Air India ilisema, "Jumla ya watu saba walioonyesha dalili kwa nyakati tofauti wakati wa safari ya ndege walipokea huduma ya kwanza ya matibabu kutoka kwa timu ya matibabu iliyokuwa ikiwasubiri baada ya kutua Mumbai. Baadaye walihamishiwa hospitalini kwa uchunguzi na wote wameruhusiwa kurudi nyumbani."
Mamlaka ya usafiri wa anga nchini India imeanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha tukio hili. Ingawa afisa mmoja wa Air India alidai kuwa huenda sababu ilikuwa "kupungua polepole kwa shinikizo la hewa ndani ya ndege (slow decompression)," mamlaka ya anga inaelekeza uchunguzi wake zaidi kwenye uwezekano wa sumu ya chakula kilichotolewa ndani ya ndege.
Sababu kuu inayopelekea mamlaka kuzingatia uwezekano wa sumu ya chakula ni kwamba marubani, ambao walipatiwa chakula kilichopikwa jikoni tofauti, hawakuonyesha dalili kama hizo walizozipata abiria na wafanyakazi wengine. Hii inazua maswali kuhusu usafi wa chakula cha kawaida kilichotolewa kwa abiria na wafanyakazi.
Zaidi ya hayo, rekodi za ndege zinaonyesha kuwa hakuna barakoa za oksijeni zilizotumika wakati wa safari, jambo linalopunguza uwezekano wa matatizo ya shinikizo la hewa na kuongeza mkazo wa uchunguzi kwenye uwezekano wa chakula kilichochafuliwa.
Mamlaka ya usafiri wa anga imesema kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi wa kina, itazingatia kuweka vikwazo zaidi kwa shirika hilo la ndege, ikiwa itabainika kuwa kuna uzembe.
Tukio hili linazidi kuongeza sintofahamu kwa Air India, hasa ikizingatiwa kuwa lakuja siku 12 tu baada ya ajali mbaya ya ndege iliyosababisha vifo vya watu 274 mnamo Juni 12. Licha ya juhudi za shirika hilo za kuboresha huduma zake za ndani ya ndege kufuatia janga hilo, tukio hili jipya linaibua tena maswali kuhusu usalama na ubora wa huduma zake.