Kampuni kubwa ya magari ya umeme, Tesla, imefungua rasmi kituo chake cha kwanza cha kipekee chenye mchanganyiko wa mgahawa na kituo cha kuchaji magari ya umeme, kinachojulikana kama 'Diner', katikati ya jiji la Los Angeles (LA), Marekani. Kituo hiki kinalenga kutoa huduma kamili kwa madereva wa Tesla, kikiunganisha ulaji, burudani, na kuchaji magari katika eneo moja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla, Elon Musk, alitumia jukwaa la X (zamani Twitter) kutangaza uzinduzi huu mkubwa, akishiriki picha na video mbalimbali za kituo hicho. Siku moja kabla ya uzinduzi rasmi, Tesla ilitangaza kwenye akaunti yake ya X kuwa: "Tesla Diner & Supercharger sasa imefunguliwa Hollywood, LA. Inafanya kazi masaa 24, siku saba kwa wiki." Musk alishiriki ujumbe huu akiongeza kuwa, "Kama ‘Diner’ yetu yenye mchanganyiko wa mtindo wa zamani na wa kisasa itafanya vizuri kama ninavyofikiri, Tesla itajenga vituo kama hivi katika miji mikubwa duniani kote." Alisisitiza kuwa kituo hicho ni "kisiwa chenye chakula kizuri, mazingira mazuri, na burudani, ambapo yote haya yanafanyika wakati gari lako linachaji."
Musk pia alipongeza ubora wa vyakula vinavyopatikana mgahawani hapo, ikiwemo mikate ya nyama (hamburger), wafla, hotdog, na chipsi, akifafanua kuwa viungo vyote vinatoka kwa wakulima wa ndani. Video na picha zilizosambazwa na watumiaji mbalimbali wa X zilionyesha umati mkubwa wa watu waliofurika kituo hicho siku ya kwanza, huku foleni ndefu zikishuhudiwa.
Kituo hiki, kilichojengwa kwenye eneo la mita za mraba 2023 (takriban ekari 0.5), kina vituo 80 vya kuchaji magari ya umeme ya Tesla. Pia kimefungwa skrini mbili kubwa za kuonyesha filamu na burudani nyinginezo kwa wageni wanaosubiri. Ndani ya duka, kuna bidhaa mbalimbali zinazohusiana na Tesla zinazouzwa. Hii inaakisi mtindo wa Tesla wa kuunganisha teknolojia na uzoefu wa mteja, jambo ambalo linaweza kuleta mageuzi katika sekta ya magari ya umeme duniani kote, ikiwemo Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki ambako matumizi ya magari ya umeme bado yapo katika hatua za awali.
Moja ya vivutio vikubwa vilivyoshuhudiwa katika picha na video kutoka eneo hilo ni kuonekana kwa roboti ya kisasa ya Optimus, ambayo Tesla inaendeleza, ikitoa popcorn kwa wateja kwenye kibanda cha popcorn. Pia, masanduku ya chakula yaliyotumika mgahawani yamebuniwa kwa umbo la lori la kubeba mizigo la Tesla, Cybertruck, jambo lililovutia wengi. Hatua hii ya Tesla inaweza kuhamasisha wawekezaji nchini Tanzania kuchunguza fursa za kujenga vituo vya kisasa vya kuchaji magari ya umeme, na hata kuunganisha huduma mbalimbali ili kuboresha uzoefu wa watumiaji wa magari ya umeme.