Sayansi ya Ajabu: Dunia Inazunguka kwa Kasi, Siku Zinakuwa Fupi Zaidi

it | Thu Jul 10 2025


Sayansi ya Ajabu: Dunia Inazunguka kwa Kasi, Siku Zinakuwa Fupi Zaidi

Wanasayansi wamebainisha jambo la kipekee linalotarajiwa kutokea katika miezi ya Julai na Agosti mwaka huu. Kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Vipimo ya Australia (NMI), mzunguko wa Dunia unatarajiwa kuongezeka kasi, na kusababisha baadhi ya siku kuwa fupi kuliko kawaida kwa takriban milisekunde moja, ambayo ni sawa na sehemu moja ya elfu ya sekunde. Hasa, tarehe 9 na 22 Julai, pamoja na 5 Agosti, zinatajwa kuwa miongoni mwa siku zitakazoathirika.


Ingawa tumezoea dhana kwamba siku ina saa 24, sawa na sekunde 86,400, uhalisia wa kisayansi unaonyesha kuwa mzunguko wa Dunia si thabiti kama sheria tulizojiwekea. Kasi ya mzunguko huu hubadilika-badilika kutokana na nguvu mbalimbali, ikiwemo mvuto wa Mwezi, mikondo ya hewa katika angahewa, na mabadiliko ya kimsimu.


Kwa mamilioni ya miaka, mvuto wa Mwezi umekuwa na athari ya kuchelewesha mzunguko wa Dunia. Mvuto huu huvuta maji ya bahari na kusababisha msuguano kati ya maji na sakafu ya bahari, jambo linalotumia nishati ya mzunguko wa Dunia na kuifanya ipungue kasi polepole. Hii ndiyo sababu, kihistoria, urefu wa siku umekuwa ukiongezeka kidogo kidogo kwa kipindi kirefu.


Hata hivyo, wanasayansi wamegundua mwelekeo wa kushangaza tangu mwaka 2020. Badala ya kupungua kasi, mzunguko wa Dunia umeanza kuongezeka kasi kidogo. Sababu kamili ya ongezeko hili bado haijabainika wazi. Rekodi ya siku fupi zaidi kuwahi kurekodiwa ilikuwa mwaka jana, tarehe 5 Julai, ambapo siku ilikuwa fupi kwa milisekunde 1.66. Ongezeko hili la kasi linaonekana kuwa la kimsimu, ambapo Dunia huzunguka haraka zaidi katika kipindi cha Julai-Agosti na kupunguza kasi kati ya Novemba na Machi, kutokana na jinsi mikondo ya hewa na bahari inavyosonga.


Mabadiliko haya huathiri muda unaopimwa kulingana na mzunguko halisi wa Dunia, unaojulikana kama Saa za Kiastronomia (UT1). Hata hivyo, hayaathiri mifumo ya teknolojia tunayoitumia, ambayo inafuata Saa Sanifu ya Kimataifa (UTC). UTC ni mfumo thabiti usiotegemea mzunguko wa Dunia, bali unapima muda kwa kutumia mtetemo sahihi wa atomi za ‘caesium’.


Ili kuweka uwiano kati ya UT1 na UTC, mfumo wa "sekunde rukia" (leap second) ulianzishwa mwaka 1972. Mfumo huu uliruhusu kuongeza sekunde moja kwenye saa za dunia pale tofauti kati ya mifumo hiyo miwili ilipofikia sekunde 0.9. Hadi sasa, sekunde rukia zimeongezwa mara 27, lakini mamlaka za kimataifa zimekubaliana kuacha utaratibu huu ifikapo mwaka 2035. Hii ni kutokana na hofu kwamba mabadiliko ya ghafla ya sekunde moja yanaweza kusababisha matatizo kwenye mifumo nyeti inayohitaji usahihi wa hali ya juu kama vile GPS, mifumo ya kifedha, na biashara za mtandaoni.


Licha ya mabadiliko haya ya kisayansi, wataalamu wanasisitiza kuwa wananchi wa kawaida hawataona wala kuhisi tofauti yoyote. Michael Waters, mkuu wa kitengo cha muda katika NMI, alisema, "Tofauti ya milisekunde moja ni ndogo mno kwa ubongo wa binadamu kuitambua. Hata kama tofauti hii ikijumlisha na kufikia sekunde kadhaa kwa miaka 100, bado hakuna atakayegundua."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.