Katika maisha ya kila siku, saa janja (smartwatch) zimekuwa zikipata umaarufu kama vifaa vya mitindo na kurahisisha mawasiliano. Hata hivyo, utafiti mpya wa kisayansi unapendekeza kuwa saa hizi zinaweza kuwa na jukumu kubwa zaidi: kuwa mstari wa mbele katika kuzuia kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile UVIKO-19 na mafua makali.
Watafiti kutoka vyuo vikuu vya Texas A&M na Stanford nchini Marekani wamegundua kuwa teknolojia hii inaweza kubaini dalili za awali za ugonjwa ndani ya saa 12 tu baada ya mtu kuambukizwa. Hii inamaanisha kuwa saa yako inaweza kukupa tahadhari ya ugonjwa hata kabla wewe mwenyewe hujisikia mgonjwa.
Siri ya uwezo huu iko katika jinsi saa janja zinavyofuatilia taarifa muhimu za mwili wako bila wewe kujua. Vifaa hivi hupima na kurekodi mabadiliko madogo madogo katika mapigo ya moyo, kiwango cha oksijeni kwenye damu, mpangilio wa usingizi, na hata joto la mwili. Kwa mfano, ongezeko dogo la joto la mwili au mabadiliko yasiyo ya kawaida katika ubora wa usingizi wako yanaweza kuwa ishara ya kwanza kwamba mfumo wako wa kinga umeanza kupambana na maambukizi.
Umuhimu wa ugunduzi huu unatokana na ukweli kwamba magonjwa mengi, ikiwemo UVIKO-19, husambazwa na watu wasioonyesha dalili (asymptomatic). Utafiti wa awali ulionyesha takriban asilimia 44 ya maambukizi ya Corona yalisababishwa na watu waliokuwa katika hatua za awali za ugonjwa bila wao kujijua. Kwa kutoa tahadhari mapema, saa janja inaweza kumfanya mtu achukue hatua za haraka, kama vile kujitenga kwa hiari na kufanya vipimo, na hivyo kuzuia kuwaambukiza wengine.
Ili kuthibitisha hili, watafiti walitumia mifumo ya hisabati kuiga hali halisi. Matokeo yao yalikuwa ya kushangaza: iwapo watu waliopokea tahadhari kutoka kwenye saa zao wangepunguza mwingiliano na wengine kwa asilimia 66, kasi ya maambukizi (inayopimwa kwa Kima cha Maambukizi-R) ya UVIKO-19 na mafua makali ingepungua kwa nusu. Na endapo mwingiliano ungepunguzwa kwa asilimia 75, mlipuko wa magonjwa hayo ungeweza kusitishwa kabisa.
Profesa Martial Ndeffo, mmoja wa watafiti wakuu, alieleza kuwa watu wengi hupuuza dalili za awali kama vile uchovu na kuendelea na shughuli zao. "Lakini iwapo saa yako itakupa taarifa kuwa kuna uwezekano mkubwa una maambukizi, itakupa msukumo wa kuchukua hatua," alisema. Teknolojia hii inaweza pia kutumika kwa magonjwa mengine ya mfumo wa hewa kama vile RSV.
Ili teknolojia hii iweze kutumika kama zana halisi ya afya ya umma, hasa katika maeneo kama Tanzania, bado kuna changamoto za kushughulikia, ikiwemo upatikanaji na gharama za saa hizi, pamoja na umuhimu wa kuweka mikakati ya kuhamasisha wananchi kuzitumia na kulinda faragha ya taarifa zao za kiafya.