UVIKO-19 Bado Upo, Tahadhari Yaendelea Kuhitajika - Dk. Magembe

culture | Tue May 20 2025


UVIKO-19 Bado Upo, Tahadhari Yaendelea Kuhitajika - Dk. Magembe

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, akieleza kuwa ugonjwa huo bado upo nchini kwa kiwango cha chini, sawa na magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa njia ya hewa.


Katika taarifa yake aliyoitoa leo, Dk. Grace amesema kuwa vipimo vya maabara vimegundua kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza, hali ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika miaka iliyopita na inajulikana kama 'Seasonal influenza'. Alifafanua kuwa vipimo hivyo vimeonyesha kuwa hakuna kirusi kipya kilichogunduliwa.


Amebainisha kuwa kuanzia mwezi Februari hadi Aprili mwaka huu, ufuatiliaji wa virusi umeonyesha ongezeko la visa vya UVIKO-19. Mwezi Februari, kulikuwa na wagonjwa wawili kati ya watu 139 waliopimwa (asilimia 1.4), na idadi hiyo iliongezeka hadi wagonjwa 31 kati ya watu 190 waliopimwa mwezi Machi (asilimia 16.3). “Mwezi Aprili mwaka huu, kulipatikana wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa, sawa na asilimia 16.8. Hali hii ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa imekuwa ikitokea kila mwaka tangu UVIKO-19 ulipotangazwa kwa mara ya kwanza mwaka 2020,” alieleza Dk. Grace.


Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki, ongezeko la visa linaonekana zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam. Hata hivyo, alihakikisha wananchi kuwa Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa nchini na itatoa taarifa zaidi inavyobidi.


Ushauri wa Dk. Magembe kwa wananchi ni kuendelea kuzingatia kanuni za afya, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, na kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya njia ya hewa. Ingawa kiwango cha maambukizi kwa sasa ni cha chini, bado ni muhimu kwa kila mmoja kuwa na tahadhari ili kuepusha kuenea zaidi kwa virusi vya UVIKO-19 na magonjwa mengine ya mfumo wa upumuaji.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.