Meta Yafungua 'Gym' ya Bei Chee kwa AI: Sasa Roboti Watajifunza Bila Kuvunja Benki wala Kuharibu Vitu

it | Fri Nov 21 2025


Meta Yafungua 'Gym' ya Bei Chee kwa AI: Sasa Roboti Watajifunza Bila Kuvunja Benki wala Kuharibu Vitu

Katika ulimwengu wa teknolojia, kufundisha Akili Mnemba (AI) au roboti kufanya kazi ngumu ni ghali na hatari kama kumpa mtoto gari la kifahari ajifunze kuendesha barabarani. Lazima atagonga, ataharibu, na gharama zitakuwa kubwa. Kwa muda mrefu, makampuni yamekuwa yakihangaika na gharama hizi za "kujaribu na kukosea" (trial and error) zinazohitajika katika mafunzo ya AI, kitaalamu yakiitwa Reinforcement Learning (RL).


Lakini sasa, kampuni ya Meta (wamiliki wa Facebook na Instagram), wakishirikiana na watafiti wabobezi kutoka Chuo Kikuu cha Chicago na UC Berkeley, wamekuja na suluhisho la 'kimasikini' lenye matokeo ya 'kitajiri'. Wamezindua mfumo mpya uitwao 'DreamGym'.


DreamGym ni Nini?


Fikiria unataka kumfundisha bondia. Badala ya kumpeleka ulingoni apigwe ngumi za kweli na kuumizwa ili ajifunze kukwepa, unamweka kwenye 'gym' ya kisasa ambapo anapigana na vivuli au mashine ambazo hazimuumizi lakini zinamfundisha mbinu zote. DreamGym inafanya hivyohivyo kwa AI.


Ni mazingira ya kidijitali (virtual environment) ambapo "Mawakala wa AI" (AI Agents) wanaweza kujifunza kutatua matatizo, kufanya maamuzi, na kupanga mikakati bila kugusa ulimwengu wa kweli.


Tatizo Lililokuwepo


Zamani, ili AI ijifunze jinsi ya kununua bidhaa mtandaoni au kuendesha mtambo kiwandani, ilibidi ijaribu kwenye mifumo halisi au itengenezewe mazingira magumu sana ya kuiga (simulators) ambayo ni ghali kutengeneza. Kwenye mifumo halisi, AI ikikosea inaweza kufuta faili muhimu, kununua vitu visivyotakiwa, au kuharibu mashine.


Jinsi DreamGym Inavyofanya Kazi: Uchawi wa Maneno


Tofauti na mifumo mingine inayotumia picha nzito za video (kama magemu ya Playstation) kufundisha AI, DreamGym inatumia maandishi (text) kuunda ulimwengu wa kufikirika.


Inafanya kazi kwa kutumia nguzo kuu tatu:


  1. Kufikiria Mazingira (Reasoning-based Model): AI inajenga picha ya kinachoendelea kwa kutumia maelezo ya maandishi. Kwa mfano, badala ya kuonyesha picha nzima ya tovuti ya manunuzi, inaambiwa "hiki ni kitufe cha kulipa, hiki ni kapu la bidhaa." Hii inapunguza sana hitaji la data na nguvu ya kompyuta.
  2. Kumbukumbu ya Mazoezi (Replay Buffer): Inahifadhi makosa na mafanikio ya nyuma ili AI isirudie kosa lilelile.
  3. Mwalimu Mwenye Akili (Curriculum Generator): Hii ni sehemu inayotunga mitihani. Inahakikisha AI haipewi kazi ngumu ghafla. Ikishafahamu kazi rahisi, "mwalimu" huyu anaongeza ugumu kidogo kidogo (curriculum) ili kuikomaza AI.


Matokeo ya Kushangaza


Kwenye majaribio yaliyofanywa kwa kutumia mifumo ya Llama 3 na Qwen 2.5, matokeo yamekuwa ya kufurahisha sana.


  1. Kasi na Ufanisi: Katika mazingira magumu ya wavuti (WebArena), DreamGym iliongeza ufanisi kwa zaidi ya asilimia 30 ukilinganisha na njia za zamani.
  2. Uhamisho wa Maarifa: Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa AI iliyojifunza kwenye DreamGym iliweza kuchukua ujuzi ilioupata kwenye kazi moja (kama duka la mtandaoni) na kuutumia kwenye kazi nyingine tofauti kabisa. Hii inaonyesha kuwa AI haikukariri tu, bali ilielewa "kanuni za kazi."
  3. Gharama Nafuu: Watafiti wamethibitisha kuwa kwa kutumia DreamGym, makampuni yanahitaji data halisi (real data) chache sana—chini ya asilimia 10 ya ilivyozoeleka. AI inajifunza mengine yote kwenye 'ndoto' zake (simulation) na kisha inapoamka (kuja kwenye ulimwengu halisi), inafanya kazi kwa ufanisi wa asilimia 40 zaidi kuliko iliyofundishwa kienyeji.


Hii ni habari njema kwa wabunifu wa programu na makampuni machanga (startups) hata hapa Tanzania, kwani inaashiria kuwa huko tuendako, kuunda AI yenye akili hakutahitaji mabilioni ya fedha wala seva kubwa kama za Google, bali ujanja wa kutumia zana kama DreamGym.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.