Kuna msemo wa wahenga usemao, "Kufa kufaana." Wakati kampuni kubwa ya Marekani ya Nvidia ikilia kwa uchungu baada ya serikali ya Washington kuweka vikwazo vikali vya kutosafirisha vipuri vya kompyuta (Chips) kwenda China, kampuni ya teknolojia ya Baidu imeona hiyo ni fursa ya dhahabu ya kutawala soko la nyumbani.
Baidu, ambayo inajulikana na Watanzania wengi kama "Google ya China" kutokana na injini yake ya utafutaji (Search Engine), sasa imegeuza mwelekeo wake kibabe. Imeamua kuwekeza nguvu zote kwenye ulimwengu wa Akili Mnemba (AI) na magari yanayojiendesha, ikilenga kuziba pengo lililoachwa na Marekani katika soko la China.
Roadmap ya Miaka 5: Mipango Mikakati
Kupitia kampuni yake tanzu iitwayo Kunlunxin, Baidu imeanika mpango mkakati wa miaka mitano unaolenga kuifanya China isitegemee tena teknolojia ya nje. Ripoti kutoka CNBC zinaeleza kuwa kampuni hiyo itazindua kizazi kipya cha chipu za AI ziitwazo ‘M100’ ifikapo mwaka 2026, na kufuatiwa na toleo la ‘M300’ mwaka 2027.
Hizi si chipu za kawaida; ndizo zinazotumika kuendesha mtambo wa AI wa Baidu uitwao 'Ernie Bot' (ambao ni mshindani wa ChatGPT nchini China). Lengo la Baidu ni kuwa na "Full Stack AI Platform"—yaani wamiliki kila kitu kuanzia uzalishaji wa vipuri, ujenzi wa seva, hadi programu za mwisho zinazotumiwa na mwananchi.
Pesa Nje Nje: Wachumi Watabiri Neema
Wachambuzi wa masuala ya fedha duniani wameanza kuona nyota ya Baidu iking'aa. Benki ya JP Morgan imetabiri kuwa mapato ya mauzo ya chipu za Baidu yatapaa mara sita zaidi na kufikia Yuan bilioni 8 ifikapo mwaka 2026. Ukibadilisha fedha hizi kwenda kwenye madafu yetu, ni takriban Shilingi Trilioni 3 za Kitanzania.
Vilevile, kampuni ya Macquarie imekadiria kuwa thamani ya kampuni ya Kunlunxin pekee inaweza kufikia Dola bilioni 28, ambayo ni sawa na takriban Shilingi Trilioni 75.6 za Kitanzania. Hii ni pesa ndefu sana ambayo inaonyesha imani ya soko kwa uwezo wa China kujitegemea.
Nvidia Yapigwa 'Pini', Huawei Yaelemewa
Hali halisi nchini China ni kwamba soko lina kiu kali ya vipuri vya AI. Nvidia, ambayo ndiyo kinara duniani, imezuiwa na serikali ya Marekani kuuza chipu zake zenye nguvu kubwa nchini humo. Hata lile toleo walilotengeneza maalum kwa ajili ya China (H20), serikali ya Beijing imewataka wafanyabiashara wake kupunguza kulitumia ili kukuza soko la ndani.
Mshindani mwingine wa ndani, Huawei, anajitahidi kujenga mifumo mikubwa (clusters), lakini uwezo wake wa kuzalisha haukidhi mahitaji makubwa ya soko. Hapa ndipo Baidu anapoingia kama mkombozi. Tayari wameanza kupata oda nono, ikiwemo kutoka kwa kampuni kubwa ya mawasiliano ya China Mobile.
Kilio cha Alibaba na Tencent
Uhaba wa chipu umekuwa mwiba kwa makampuni mengine makubwa ya China. Bosi wa Alibaba, Eddie Wu, amekaririwa akisema miaka miwili ijayo itakuwa migumu kutokana na ukosefu wa vipuri. Nayo Tencent imelazimika kupunguza kasi ya uwekezaji wake kwa mwaka 2025, si kwa sababu hawana pesa, bali kwa sababu hawana chipu za kutosha kununua.
Hali hii inatokana na ukweli kwamba kiwanda kikubwa cha ndani cha China, SMIC, bado hakijafikia kiwango cha kiteknolojia cha TSMC ya Taiwan, hivyo uzalishaji bado ni mdogo.
Fursa Katika Matatizo
Nick Patience, mchambuzi kutoka The Futurum Group, amesema wazi: "Vikwazo vya Marekani vimebadilisha soko la China kuwa la mabilioni ya dola kwa wazalishaji wa ndani."
Kwa Watanzania, hii ni funzo la kimkakati. China imeamua kutokubali kuyumbishwa na teknolojia ya nje. Badala ya kulalamika walipofungiwa Nvidia, wamegeuka na kuanza kujenga viwanda vyao. Baidu sasa inajiandaa kuwa "Intel au Nvidia mpya ya Asia," ikithibitisha kuwa penye nia pana njia, na vikwazo vinaweza kuwa chachu ya maendeleo ya ndani.