Marekani Yataka Kuzipiga 'Pini' Alibaba, BYD na Baidu, Yadai ni 'Mashushushu' wa Jeshi la China

it | Fri Nov 28 2025


Marekani Yataka Kuzipiga 'Pini' Alibaba, BYD na Baidu, Yadai ni 'Mashushushu' wa Jeshi la China

Wakati wafanyabiashara wa Kariakoo na Watanzania wengi wakiendelea kutegemea mtandao wa Alibaba kuagiza bidhaa, na wakati magari ya umeme ya BYD yakianza kutamaniwa barabarani, hali ya hewa kati ya Marekani na China imezidi kuchafuka. Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imefikia hitimisho zito na la hatari kibiashara kwamba kampuni kubwa za teknolojia za China—Alibaba, Baidu, na BYD—zinapaswa kuingizwa kwenye orodha ya makampuni yanayolisaidia Jeshi la China (PLA).


Hatua hii imekuja kama radi katikati ya mvua, ikitishia kuzorotesha uhusiano wa kibiashara na kuweka kampuni hizo maarufu katika hatari ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi (Blacklist) na taifa hilo lenye nguvu duniani.


Pentagon Yawasha Taa Nyekundu


Kwa mujibu wa ripoti za kiintelijensia zilizochapishwa na Bloomberg, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Stephen Feinberg, aliandika barua nzito kwenda Bunge la Marekani (Congress) mnamo Oktoba 7, akiwasilisha majina ya kampuni nane mpya zinazodaiwa kuwa na mafungamano ya siri na jeshi la China.


Katika orodha hiyo, majina makubwa yaliyowashitua wengi ni:


  1. Alibaba: Jukwaa kubwa la biashara ya mtandaoni linalotumiwa na mamilioni duniani.
  2. Baidu: Kampuni inayojulikana kama "Google ya China" kutokana na injini yake ya utafutaji na teknolojia ya AI.
  3. BYD: Kampuni inayoongoza duniani kwa sasa katika utengenezaji wa magari ya umeme (EV), ikichuana vikali na Tesla ya Elon Musk.


Mbali na vigogo hao watatu, kampuni nyingine zilizotajwa ni pamoja na Eoptolink Technology, Hua Hong Semiconductor, RoboSense Technology, WuXi AppTec, na Zhongji Innolight. Hizi ni kampuni zinazojihusisha na utengenezaji wa chipu, sensa za roboti, na teknolojia za hali ya juu.


Orodha ya '1260H' ni Nini?


Marekani ina sheria maalum inayojulikana kama 'Section 1260H'. Hii ni orodha inayotolewa kila mwaka ikianika makampuni ambayo Marekani inaamini yanatumika kama "kivuli" cha Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA).


Kuingizwa kwenye orodha hii hakumaanishi kufungiwa biashara papo hapo, lakini ni sawa na kupewa "Kadi ya Njano" kwenye soka. Ni onyo kali kwa wawekezaji wa Marekani na mashirika ya kimataifa kuwa kufanya biashara na kampuni hizi ni hatari kwa usalama wa taifa la Marekani. Hii inaharibu sifa (Reputation) ya kampuni na mara nyingi ni hatua ya awali kabla ya Wizara ya Biashara ya Marekani haijatoa "Kadi Nyekundu" (Entity List) ambayo huzuia kabisa kampuni hizo kununua teknolojia ya Marekani au kufanya biashara nchini humo.


Ikumbukwe kuwa mwezi Januari mwaka huu, orodha hii ilikuwa na makampuni 134, yakiwemo majina makubwa kama Tencent (wamiliki wa WeChat) na CATL (watengenezaji wakubwa wa betri).


Siasa za 'Paka na Panya' za Trump na Xi


Kinachofanya taarifa hizi kuwa na ukakasi ni muda wa kutolewa kwake. Barua ya Feinberg iliandikwa wiki tatu tu kabla ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa China, Xi Jinping, kukubaliana kuweka "Silaha Chini" katika vita ya kibiashara (Trade Truce).


Wadadisi wa mambo ya kidiplomasia wanajiuliza: Je, hii ni mbinu ya Marekani ya kuweka shinikizo la chini kwa chini hata wakati wakicheka na China hadharani? Au ni mfumo wa serikali (Deep State) unaofanya kazi tofauti na matakwa ya kisiasa ya Rais?


Athari kwa Uchumi wa Dunia na Tanzania


Kwa Tanzania, hatua hizi za Marekani zina maana kubwa. Ikiwa Alibaba itawekewa vikwazo vikali, inaweza kuathiri mifumo ya malipo ya kimataifa au upatikanaji wa bidhaa kwa bei nafuu. Vilevile, kampuni ya BYD imekuwa ikitegemewa kuleta mapinduzi ya magari ya umeme barani Afrika kwa bei rafiki. Ikiwa itapigwa "pini" na Marekani, huenda upatikanaji wa vipuri na teknolojia ukawa mgumu, au bei ikapanda.


Hata hivyo, mpaka sasa Wizara ya Biashara ya Marekani haijatangaza rasmi kuzifungia kampuni hizi, lakini "moshi ukitoka, moto upo chini." Dunia inasubiri kuona je, majina haya yataonekana rasmi kwenye orodha mpya itakayotolewa mwakani?

Kama wahenga wasemavyo, "Fahari wawili wapiganapo, ziumiazo ni nyasi." Vita hii ya kiuchumi kati ya Marekani na China inaendelea kuweka biashara za kimataifa, ikiwemo za wafanyabiashara wetu, katika njia panda.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.