Kuna msemo wa wahenga unaosema, "Wanaovujisha ngoma ndio waanzilishi wa kuicheza," lakini katika ulimwengu wa soko la hisa, inaonekana waanzilishi sasa wameamua kuondoka kimpya kimpya kabla ngoma haijapasuka. Hali ya wasiwasi imeanza kutanda kwa wawekezaji wadogo duniani kote baada ya ripoti mpya kuonyesha kuwa mwekezaji nguli na bilionea wa Silicon Valley, Peter Thiel, ameungana na wenzake "kuruka mtumbwi" wa kampuni ya NVIDIA.
Peter Thiel, ambaye anafahamika kwa uwezo wake wa kipekee wa kunusa fursa (akiwa mmoja wa wawekezaji wa kwanza kabisa wa Facebook na mwanzilishi wa PayPal), kupitia mfuko wake wa uwekezaji wa 'Thiel Macro', ameripotiwa kuuza hisa zake zote alizokuwa nazo katika kampuni ya NVIDIA.
Kwanini Wanauza Sasa?
Uamuzi huu wa Thiel kuuza hisa zipatazo 537,742, zenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani milioni 100 (sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 260), umekuja wakati ambapo hisa za NVIDIA zimefikia thamani ya juu zaidi ya historia, zikigonga soko la mtaji la Dola Trilioni 5.
Wachambuzi wa masuala ya fedha wanasema hatua hii inatafsiriwa kama imani kwamba bei ya hisa za kampuni hiyo imefika "kileleni" (peak) na haiwezi kupanda zaidi ya hapo, au mbaya zaidi, puto la uwekezaji linaweza kupasuka muda wowote. Thiel sasa ameamua kubaki na hisa zake katika makampuni mengine makubwa kama Apple, Microsoft, na Tesla, akiiacha NVIDIA ikiwa haina mtetezi kwenye mfuko wake.
Hii inakuja siku chache tu baada ya kampuni kubwa ya uwekezaji ya Japani, SoftBank, nayo kufanya uamuzi mgumu wa kuuza hisa zake zote za NVIDIA zilizokuwa na thamani ya Dola bilioni 5.83 (takriban TZS Trilioni 15.1). Kitendo cha makampuni haya mawili makubwa kuuza hisa zao kwa mpigo kimezua maswali mengi: Je, wanajua kitu ambacho sisi hatukijui?
Soko Lagawanyika
Licha ya vigogo hawa kuondoka, soko la hisa bado limegawanyika. Ripoti zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Septemba, kati ya mifuko 909 ya uwekezaji (Hedge Funds), 161 iliongeza uwekezaji wao kwa NVIDIA, huku 160 ikipunguza au kuondoa kabisa. Hii ni "sare" inayochanganya, inayoashiria kuwa vita ya kubashiri mustakabali wa NVIDIA ni kali.
Hata hivyo, soko liliitikia kwa mshtuko kidogo, huku hisa za NVIDIA zikishuka kwa asilimia 3 katika soko la New York baada ya habari hizi kusambaa, zikifuta faida ndogo iliyokuwa imepatikana tangu mwishoni mwa Septemba.
Pesa Inahamia Kwa Google
Wakati NVIDIA ikianza kuwatia hofu wawekezaji, "Babu" wa uwekezaji duniani, Warren Buffett, ameonyesha mwelekeo mpya. Kampuni yake ya Berkshire Hathaway imeripotiwa kumwaga kiasi cha Dola bilioni 4.9 (takriban TZS Trilioni 12.7) kununua hisa za Google (Alphabet).
Hatua hii ya Buffett, ambaye kwa kawaida hapendi sana kuwekeza kwenye makampuni ya teknolojia yanayobadilika haraka, imeongeza imani kubwa kwa Google na kusababisha hisa zake kupanda kwa asilimia 6 na kufikia kiwango cha juu cha historia. Hii inaashiria kuwa "pesa ndefu" (smart money) sasa inahama kutoka kwa watengenezaji wa 'chip' (kama NVIDIA) na kuelekea kwa wamiliki wa data na mifumo ya AI (kama Google).
Kwa Mtanzania anayefuatilia masuala ya uchumi, funzo hapa ni kwamba katika uwekezaji wa teknolojia, upepo hubadilika haraka sana. Wakati mwingine, "kuuza wakati wa shangwe" ndiyo siri ya matajiri wakubwa kulinda utajiri wao.